Header Ads Widget

SABA WAJITOKEZA KUWANIA UENYEKITI WA HALMASHAURI YA HAI



WAKATI pazia la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea umeya na uenyekiti wa halmashauri likiwa limefungwa rasmi jana, madiwani wateule saba ‘wanakesha’ Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, kusubiri uamuzi wa chama hicho.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Hai, Kumotola Kumotola, alisema jana kuwa madiwani hao saba, ndio walikuwa wamechukua fomu hadi kufikia Novemba 4, mwaka huu, huku wengine watano wakijitosa kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti.

“Mwisho ilikuwa jana Novemba 4, majira ya saa 10:00 jioni. Hivi sasa tunaanza vikao vya kuwajadili wagombea hao kwa ngazi ya wilaya na baadaye tutapeleka mapendekezo yetu mkoani ili kuwapa nao nafasi ya kuanza vikao ngazi ya mkoa,” alisema Kumotola.

Wanaotunishiana msuli katika nafasi hiyo na kata zao kwenye mabano ni Edmund Rutaraka (Muungano), Evod Njau (Bomang’ombe) na Martin Munisi (Machame Magharibi).

Wengine waliojitosa kugombea ni John Lengai (Narumu), Jublate Ndossi (Masama Mashariki), Kandaka Kimaro (Masama Kati) na Kehela Kipara (KIA).

Nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hadi 2020, ilikuwa ikishikiliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kwa mujibu wa ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Tanzania, Serikali za Mitaa ni vyombo vya haki na vyenye mamlaka ya kushiriki na kushirikisha wananchi katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma katika sehemu zao.

Serikali za Mitaa huanzishwa kwa madhumuni ya kuwahudumia wananchi na kuwapelekea madaraka, kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Kazi za jumla na za lazima za serikali za mitaa, ziko katika Sheria za Serikali za Mitaa Sura 287 na 288, Toleo la 2002. Awali kabla ya mapitio, zilikuwa chini ya Sheria Namba 7 na 8 za Mwaka 1982.

Post a Comment

0 Comments