Header Ads Widget

MAGONJWA YA KIPINDUPINDU NA KUHARA YAPUNGUA KWA ASILIMIA MBILI WISHITELEJA WILAYANI KISHAPU


Mtoto akicheza kwenye taka ambazo zinaweza kuhatarisha afya yake ikiwemo kupata magonjwa ya kuhara na Kipindupindu (Picha na Mtandao)

 Na Shaban Njia -Kishapu

MAGONJWA ya kipindupindu na kuhara katika kijiji cha Wishiteleja Kata ya Mondo,Halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga, wamepungua kwa asilimia mbili kutoka asilimia 18 baada ya wananchi kupewa elimu juu ya umuhimu wa unawaji mikono kabla na baada ya kutoka maliwato.

Maganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mondo, Christian Ngowi aliyabainisha hayo jana wakati akitoa taarifa ya uboreshaji huduma za lishe katika kuimarisha afya ya mama na mtoto (ENRICH) unatotekelezwa katika wilaya tano za Mikoa ya Shinyanga na Singida na World Vision Tanzania kwa ufadhiri wa serikali ya Canada.

Alisema kuwa, kabla ya kuwapatia elimu ya unawaji wa mikono, magonjwa yaliyokuwa yakiripotiwa katika Zahanati ya Mondo yalikuwa ya mlipuko hasa kipindupindu na kuhara kwa watoto chini ya miaka mitano ambapo ugonjwa huo unasababishwa na uchafuzi wa Mazingira majumbani.

Aidha Ngowi alisema,ugonjwa huo ulifika mpaka asilimia 18 sawa na watoto wadogo chini ya miaka mitano zaidi ya 216 nakwamba baada ya kutoa elimu ya umuhimu wa kunawa mikono kabla ya kufanya shughuli yoyote ugonjwa huo umeshuka hadi asilimia mbili kwa mwezi.

“Kata hii inawatoto zaidi ya 1190 chini ya miaka mitano,wengi waliokuwa wakiripotiwa Zahanati walikuwa wakiumwa ugonjwa wa kipindipindu na kuhara na hii nikwasababu ya mazingira machafu nyumbani hasa mama kumshika mtoto na kumnyonyesha kabla ya kunawa mikono au baada ya kutoka maliwato,” Alisema Ngowi.

Aliongeza kwa kueleza kuwa utoaji wa elimu wa kunawa mikono mtaa kwa mtaa umesaidia kupunguza magonjwa hayo kwa silimia mbili kutoka asilimia 18 ya hapo awali, na bado elimu inaendelea kutolewa hasa pale wanapofika klinik kwenye chanjo sambamba na utoaji wa elimu ya lishe.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri Wilaya ya Kishapu, Dkt. Shani Josephati alisema kuwa, asilimia 64 ya kaya zilizopo ndani ya Halmashauri hiyo zina vyoo bora na vya kisasa na ni baada ya utoaji wa elimu ya umuhimu wa vyoo kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania. 
 
Hata hivyo alisema kuwa, wamehakikisha magulio na minada iliyopo ndani ya Halmashauri inakuwa na huduma za vyoo nakwamba changamoto wanayokutana nayo ni wananchi kujisaidia nje ya vyoo au vichakani baada ya kuwepo huduma ya kulipia kabla ya kuingia maliwatoni.

Pia Josephati, aliwataka wananchi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kila mmoja anakuwa na choo, kunawa mikono kabla ya shughuli yoyote majumbani hasa wakati wa kunyonyesha ili kuendelea kujikinga na magonjwa ya mlipuka ambayo ni hatari kwa afya za watoto wadogo. 


OFISA Kilimo wa Kata ya Mondo,Halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga Pius Maganga aliyevaa tisheti ya blue jana akitoa elimu ya namna ya kulima bustani ya viazi lishe katika moja ya bustani za lishe inayopo kijiji Wishiteleja,pembeni ni akinamama 22 wenye watoto walio na utapiamlo (Picha na Shaban Njia)

Post a Comment

0 Comments