Header Ads Widget

WAZIRI AAGIZA WAKULIMA WA KAHAWA KARAGWE KULIPWA SH BILIONI 7.8

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Karagwe wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Kagera Leo tarehe 3 Septemba 2020.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kagera
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amekiagiza Chama Kikuu cha Ushirika Karagwe mkoani Kagera (KDCU) kuwalipa wakulima malipo yao ambapo ametoa siku tatu kuanzia leo Septemba 4, 2020 mpaka Septemba 6, 2020 jumla ya Sh. Bilioni 7.8 ziwe zimelipwa haraka.

Mhe. Hasunga alitoa agizo hilo baada ya kuwasili wilayani Karagwe  Septemba 3, 2020 kwa ziara ya kikazi ya siku moja, ambapo alikagua shughuli mbalimbali za kilimo kisha kukutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa vyama vya Ushirika (AMCOS) wa Wilaya ya Kyerwa na Karagwe ambapo amejionea hali ya malipo ya wakulima wa kahawa wanaodai.

“Ninyi KDCU ndio mmechukua kahawa za wakulimaa mmechukua kwa malikauli wananchi wakawaamini na kuwapa kahawa lakini mkawapa maneno mazuri kwamba mtawalipa kwa wakati lakini mmeshindwa kuwalipa mpaka sasa” Amesema Waziri Hasunga.

Ametoa maagizo hayo mbele ya Kamati ya ulinzi na usalama pamoja na wataalamu wa Wilaya ya Karagwe huku akikitaka Shirika la ukaguzi wa hesabu za vyama vya Ushirika (COASCO) kukamilisha ukaguzi wa vyama vya Ushirika ndani ya wiki mbili ili wakulima waweze kulipwa fedha zao za malipo ya nyongeza, Kadhalika ameitaka COASCO kupitia hesabu zao ili waweze kutoa taarifa.

Hasunga amesema kuwa ni marufuku kuchelewesha malipo ya wakulima badala yake Bodi ya Kahawa kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania inapaswa kubainisha njia bora ili kurahisisha malipo ya wakulima.

Vilevile, Waziri Hasunga ameitaka Bodi ya kahawa kujenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuhamasisha unywaji wa kahawa wa ndani kwani kufanya hivyo kutaongeza soko la ndani la kahawa.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akikagua kahawa ya wakulima katika kiwanda cha Kamahungu kinachomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Karagwe (KDCU) wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Kagera Leo tarehe 3 Septemba 2020. 
Viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa wakimsikiliza Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wakati akizungumza kwenye mkutano uliofanyika Mjini Karagwe wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Kagera Leo tarehe 3 Septemba 2020. 
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Kagera Leo tarehe 3 Septemba 2020.