Header Ads Widget

WAWILI WAUAWA KWA MAWE KAHAMA WAKIDAIWA KUVAMIA NA KUNYANG'ANYA SH MILIONI 1.75


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba

Na Damian Masyenene -Shinyanga
WATU Wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi ambao bado majina yao hayajafahamika wameuawa kwa kurushiwa mawe  na wananchi katika eneo la Manzese Kata ya Busoka Mjini Kahama mkoa wa Shinyanga, baada ya kuvamia duka la M-Pesa na kufyatua baruti hewani.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari leo Septemba 9, 2020 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, tukio hilo lilitokea jana Septemba 8 saa 2:30 usiku, ambapo baada ya majambazi hao kuvamia duka hilo na kufyatua baruti hewani walimshambulia kwa kumpiga mabapa ya panga mgongoni mmiliki wa kibanda cha M-Pesa, Paulo Charles Inena (32) kisha kumnyang'anya pesa za mauzo Sh 1,750,000.

"Majambazi hao walijaza baruti kwenye maganda yaliyotumika na kuyalipua kwa kutumia silaha aina ya shortguni, wananchi waliokuwa eneo hilo walifanikiwa kuwarushia mawe majambazi hao sehemu mbalimbali za miili yao na kusababisha mauaji hayo. 

"Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya halmashauri mji wa kahama kwa utambuzi. Kwenye eneo la tukio hilo ilipatikana silaha moja aina ya shortgun ambayo imekatwa kitako na mtutu, maganda matatu ya short gun yalitumika kujazia baruti, vocha tisa za Halotel za Sh 1000, na tano za Sh 500, vocha saba za Vodacom za Sh1000 na saba za Sh 500, vocha saba za Airtel za Sh 1000 na simu moja aina ya Tecno," amesema Kamanda Magiligimba. 

ACP Debora Magiligimba ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kutoa taarifa mara tu wanapo baini viashiria vyovyote vya uhalifu, ili kukabiliana na matukio ya uhalifu na wahalifu kabla ya uhalifu kutokea.