Header Ads Widget

WASHTAKIWA 57 WAACHIWA HURU GEREZA LA MKOA WA SHINYANGA


Mkurugenzi wa Mashtaka nchini  Biswalo Mganga amewaachia huru washtakiwa 57, wakiwepo wanaume 47 na wanawake 10 waliokuwa wanakabiliwa na kesi mbalimbali ambao waliokuwa wamewekwa katika gereza la Shinyanga.

 Biswalo  ameendesha zoezi hilo wakati alipotembelea gereza la Shinyanga akiwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wizara ya Katiba na Sheria.

Akizungumza katika tukio hilo Bw. Amon Mpanju amesema wametembelea gereza la Shinyanga ikiwa ni sehemu kuhakikisha mfumo wa upatikanaji haki ili kwa pamoja kuweza kuwasikiliza na kufahamu changamoto zilizoko  kwenye magereza na kuzitafutia suluhisho.

Akizungumza wakati akiwaachia huru mahabusu hao Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Biswalo Mganga amewataka mahabusu hao waliochiwa huru kuhakikisha hawarudii makosa waliyoyafanya kwa kuwa anahitaji nchi yenye amani huku akiwaeleza wazi kuwa yeyote kati yao ambae anajua hawezi kwenda kutulia na kuwa raia mwema abaki gerezani.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju amewasihi mahabusu hao walioachiwa huru wakirudi uraiani kwenda kuwa raia wema na wale waliobakia kukaa kwa amani na kuwasikiliza walezi wao gerezani huku wakifundishana wao kwa wao kutenda mema.

Awali kabla ya kuanza ziara ya kutembelea gereza hilo la Shinyanga wajumbe walipata nafasi ya kumtembelea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainabu Telack na kuzungumza nae juu ya ziara hiyo ambapo amepongeza juu ya hatua hiyo na kueleza kuwa ziara kama hizo zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali za magerezani.

Wakati wa ziara hiyo ya kutembelea magereza wajumbe wamechangia kiasi cha shilingi laki tatu (300,000/=)ambazo zimetolewa  kwa lengo la kuliwezesha gereza hilo kununua cherehani, sabuni na ving’amuzi kufuatia ombi la wafungwa hao.

Chanzo  (WWW.NPS.GO.TZ )