Header Ads Widget

WASAJILI, NGOs WATAKIWA KUWEKA MASLAHI YA TAIFA MBELE

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dkt. Oswald Masebo akizungumza na wasajili wasaidizi wa NGOs wa Mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Tanga katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wasajili hao yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi wetu
Wasajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) wamehimizwa kuzingatia maslahi ya Taifa katika kusajili mashirika yanayotaka kufanya kazi zake hapa nchini.

Wito huo umemetolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Oswald Masebo katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wasajili wasaidizi wa NGOs yaliyohusisha Mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Tanga.

Dkt. Masebo amesema wasajili
na NGOs wanazozisajili wana wajibu wa kufahamu kuwa lengo kuwaletea wananchi maendeleo yanafikiwa.

"Ni muhimu kutambua na kutetea maslahi ya Taifa, lazima kuwe na uelewa sahihi kuhusu maslahi yetu kama Taifa na nini nafasi yetu katika eneo hilo" alisema na kuongeza kuwa eneo lingine ni kutambua kuwa NGOs zinaweza kuwa ujenzi na utambulisho pekee kwa Taifa.

Awali akitoa mada kuhusu kazi za Bodi ya usajili, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa NGOs Richard Sambaiga amesema katika usimamizi na uratibu wa sekta ya NGOs mihimili mingine ni pamoja na Ofisi ya msajili na Baraza la NGOs, hivyo wasajili wasaidizi wanapaswa kufahamu.

Akifunga mafunzo hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makanza amewataka wasajili hao kuzingatia yote waliyojifunza na kukubaliana katika kutekeleza majukumu yao.

"Msingi mzima wa kuwaleta hapa pamoja na mpango kazi mliojiwekea uwape muongozo wa kufikia yale tunayotarajia. Mzingatie yote mliyojifunza na kukubaliana," alisema.

Kwa upande wa washiriki wamesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kama Wasajili Wasaidizi tofauti na mwanzo kabla hawajapata mafunzo.

"Tumejifunza mchakato mzima wa kuweza kusajili na kufuatilia utendaji wa kazi wa mashirika yasiyo ya Kiserikali" amesema Mosses Kisibo, Msajili Msaidizi wa NGOs kutoka jiji la Tanga.

Naye Juliana Kibonde, Msajili Msaidizi wa manispaa ya Ubungo amesema mafunzo haya yamewasaidia kuelewa sera, sheria na kanuni zinazoongoza Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na njia nzuri zaidi ya kusajili kwa njia ya ya mfumo wa kielektroniki.

Washiriki 28 kutoka Mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Tanga wamepata mafunzo hayo endelevu yenye lengo la kuwajengea uwezo kutekeleza majukumu yao.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makanza akizungumza na wasajili wasaidizi wa NGOs wa Mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Tanga wakati wa akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wasajili hao yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
Wasajili wasaidizi wa NGOs wa mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Tanga wakiwasikiliza watoa mada wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
Msajili wa NGOs kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya jamii Vickness Mayao akizungumza na wasajili wasaidizi wa NGOs wa Mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Tanga wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wasajili hao yaliyofanyika jijini Dar es salaam.

Picha zote na Kitengo cha mawasiliano Serikalini WAMJW