Header Ads Widget

PAZIA LA LIGI KUU BARA LAFUNGULIWA, SIMBA WAANZIA WALIPOISHIA

Wafungaji wa mabao ya Simba SC leo dhidi ya Ihefu FC, Nahodha John Bocco na Mzamiru Yassin wakipongezana baada ya kuihakikishia timu yao ushindi katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu msimu huu.

Na Shinyanga Press Club Blog
Leo Septemba 6, 2020 pazia la Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL) msimu wa mwaka 2020/2021 limefunguliwa rasmi kwa michezo kadhaa kuunguruma katika viwanja mbalimbali nchini.

Miongoni mwa michezo iliyopigwa leo mapema saa 10 jioni, ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Wekundu wa Msimbazi Simba wameanzia walipoishia msimu uliopita kwa kuendeleza wimbi la ushindi baada ya kuifunga Ihefu FC ya Mbeya mabao 2 kwa 1.

Mchezo huo umechezwa katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ambapo Simba walikuwa ugenini, mabao ya Simba yalifungwa na Nahodha John Bocco na Mzamiru Yassin huku goli la kufutia machozi la wenyeji likipachikwa na Omary Mponda.
Nahodha John Bocco akiifungia timu yake bao la kwanza

Katika michezo mingine iliyochezwa leo ambayo tayari imemalizika, Dodoma Jiji FC imeingia kwa kishindo ligi kuu na kuwa timu pekee kuanza kwa ushindi kati ya timu tatu zilizopanda daraja baada ya kuifunga Mwadui FC bao 1-0.


Vile vile, Mtibwa Sugar wamelazimishwa suluhu tasa na maafande wa Ruvu Shooting ya Pwani.

Katika mechi za mapema zilizopigwa saa 8 mchana, Namungo FC waliibuka na ushindi wa bao 1 kwa o, huku Biashara United wakiwakaribisha Gwambina FC katika Ligi Kuu kwa kichapo cha bao 1 kwa o.Picha kwa hisani ya Simba SC Tanzania