Header Ads Widget

WAGANGA WAKUU WATAKIWA KUHAKIKISHA KILA MTOTO NCHINI ANAPATA CHANJO


Waliokaa: Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Leonard Subi (katikati), Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk. Dafrossa Lyimo (kulia) na Mratibu wa Chanjo mkoa wa Mwanza, Amos Kiteleja (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari kutoka mkoa wa Shinyanga wakati wa semina juu ya huduma za chanjo iliyofanyika leo jijini Mwanza. Na mpiga picha wetu

Na Damian Masyenene 
ILI kuhakikisha kwamba Tanzania inafikia asilimia 100 ya utoaji chanjo kwa watoto, agizo limetolewa kwa Waganga wakuu wa mikoa na wilaya kufanya juhudi zote ili wamfikie kila motto anayestahili kupata chanjo. 

Ambapo lengo la mkakati huo ni kuepusha mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza kwa watoto, kwani watu wasiopata chanjo wana nafasi kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya magonjwa kulinganisha na wale waliopata chanjo. 

Agizo hilo limetolewa leo Septemba 4, 2020 jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wanahabari kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara juu ya huduma za chanjo zitolewazo nchini. 

Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Mafunzo ya Afya Kanda ya Ziwa uliopo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Mwanza, huku akiuhakikishia umma kwamba chanjo zinazotolewa ni salama na zina manufaa kwa watoto kwani imekuwa msaada kwa kupunguza vifo vya watoto. 

“Wazazi na walezi wawapatie watoto haki na wawapeleke katika vituo vya kutolea huduma wapate chanjo, kwa sababu watoto karibu 40,000 sawa na asilimia moja nchini wanakosa fursa ya kupata chanjo…..kwahiyo Waganga wakuu wahakikishe kila motto anayestahili kupata chanjo atafutwe na apate,” amesema. 

Dk. Subi ameeleza kuwa hadi sasa utoaji chanjo nchini hususan kwa watoto umefikia asilimia 99 kutoka 94 za mwaka 2014, huku uwekezaji katika vifaa tiba na vituo vya kutolea chanjo ukiongezeka, ambapo mwaka 2019/2021 imetengwa bajeti ya Sh Bilioni 30 za chanjo kutoka Sh Bilioni 10 mwaka 2014/15. 

“Kumefanyika ukarabati mkubwa wa maghala ya kuhifadhia chanjo ambao umegharimu Sh Bilioni 1.3, kununua friji ndani ya maghala hayo (Sh Milioni 450), kununua magari 74 (Sh Bilioni 7.7), friji 1,385 (Sh Bilioni 13) ambayo yamesambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya, zahanati na hospitali za wilaya, jumla ya vitendea kazi 4,300 vimenunuliwa na kusambazwa kwenye vituo kwa ajili ya ukusanyaji taarifa, kwahiyo chanjo zetu zinatolewa katika ubora wa hali ya juu,” amesema. 

Dk. Subi amebainisha kuwa baadhi ya magonjwa kama Surua, Polio na kuharisha yamekomeshwa kutokana na utoaji wa chanjo hizo, ambapo watoto takribani Milioni 2 hadi 3 wameendelea kuokolewa kila mwaka nchini kwa sababu ya utoaji chanjo salama na zilizothibitishwa. 

Naye Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk. Dafrossa Lyimo amesema kwamba mpango huo ulianzishwa mwaka 1975 ukitoa chanjo tatu pekee na sasa unatoa chanjo 9 zinazokinga magonjwa 13, ambapo lengo ni kumfikia kila mtoto kwa chanjo kwa usawa na kuongeza wigo wa utoaji huduma hiyo. 

Dk. Lyimo amefafanua kuwa imethibitishwa kitaalam kwamba chanjo ni mkakati muafaka wa kukinga jamii na magonjwa, kwani imebainika kuwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo yanasambaa kwa kasi kwenye jamii ambayo ina watu wengi ambao hawajapata chanjo. 

“Baadhi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo husababisha ulemavu na vifo, kwahiyo chanjo inabaki kuwa njia rahisi na sahihi ya kumlinda motto na kuwa na familia yenye afya….chanjo zote ni salama na zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya na shuleni,” amesema. 

Akitoa taarifa ya utekelezaji huduma za chanjo na uchanjaji kwa mkoa wa Mwanza kwa kipindi cha Januari hadi Julai, mwaka huu, Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza, Amosi Kiteleja amesema lengo la mkoa huo lilikuwa kuchanja watoto 101,283, na chanjo ya Pepopunda kwa wajawazito 107,968. 

Pia mkoa huo ulilenga kuchanga chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa mabinti 27,139, ambapo kila chanjo ilitakiwa ifikie walau asilimia 95, ambapo lengo limefikiwa kwa asilimia 99.


Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Leonard Subi (kushoto) akisisitiza jambo

 Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk. Dafrossa Lyimo akiwasilisha na kufafanua hoja mbalimbali kwa waandishi wa habari juu ya huduma za chanjo nchini

Waandisi wa habari wakifuatilia semina hiyo

Mafunzo yakiendelea kwa waandishi

 Dk. Dafrossa Lyimo akiendelea kutoa elimu ya chanjo kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga na Mara 
Mafunzo yakiendelea

 Waandishi wa habari wakiendelea kupata elimu ya huduma za chanjo nchini

 Waliokaa: Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk. Leonard Subi (katikati), Meneja wa Mpango wa taifa wa chanjo, Dk. Dafrossa Lyimo (kulia) na Mratibu wa chanjo mkoa wa Mwanza, Amos Kiteleja (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa habari kutoka taasisi mbalimbali za serikali mkoa wa Mwanza

 Dk. Subi na Meneja wa Mpango wa taifa wa Chanjo, Dk. Dafrossa pamoja Mratibu wa Chanjo Mwanza, Amosi Kiteleja wakiwa kwenye picha ya pamoja na waandishi wa habari kutoka mkoa wa Mara.

 Waandishi wa habari kutoka mkoa wa Simiyu (waliosimama) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya. Dk. Leonard Subi (katikati waliokaa), Meneja wa Mpango wa taifa wa chanjo, Dk Dafrossa Lyimo (kulia) na Mratibu wa Chanjo mkoa wa Mwanza, Amosi Kiteleja (kushoto).