Header Ads Widget

MAJINA YA WALIOKUFA BWENINI YATAJWA, BAKWATA YATOA NENO


Kaimu Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, DCF Charo Mangare akimsikiliza Muuguzi Mkuu Msaidizi wa Hospitali ya Nyakahanga, Justine Katalaiya (kulia), juu ya hali ya mmoja wa majeruhi wa ajali ya moto iliyosababisha vifo vya wanafunzi 10 baada ya ajali ya moto katika Shule ya Msingi ya Byamungu iliyoko Kata ya Itera,Wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera (Picha kwa hisani ya TimesMajira).
WAKATI Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) likiziomba mamlaka za uchunguzi ikiwamo Polisi kuharakisha kuchunguza matukio ya moto katika shule za Kiislamu nchini, majina ya wanafunzi 10 wa Shule ya Msingi Byamungu Islamic wilayani Kyerwa, waliokufa kwa moto usiku wa kuamkia juzi yametajwa.

Aidha, Bakwata imeziomba mamlaka hizo kuwashirikisha kila hatua muhimu za uchunguzi, ili kuondoa minong’ono ya chini kwa chini kuhusu matukio hayo.

Mbali ya hilo, imezishauri shule zote nchini, kuimarisha ulinzi wa ndani katika shule hizo na kuweka miundombinu bora, inayoendana na matakwa ya kanuni na sheria za nchi za kuanzisha shule za bweni ili kuepusha majanga yanayoweza kutokea na kugharimu maisha ya watu na mali.

Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma akizungumza na gazeti hili jana, alisema ipo minong’ono kwamba matukio ya moto katika shule hizo za Kiislamu ni hujuma inafanywa kuchonganisha watu wa itikadi fulani na serikali yao.

Lakini, alisema wao hawaamini jambo hilo, hivyo ili wawe na majibu ya kuridhisha kwa Waislamu nchini, mamlaka ziharakishe uchunguzi.

“Hatujui ni hujuma kutuchonganisha na serikali au ni vipi kwa kuwa sisi tumejipambanua wazi wazi kuunga mkono juhudi za maendeleo, amani na utulivu zinazofanywa na serikali.

Sasa ikiwa haya yanazungumzwa, pengine kweli kuna mtu nyuma ana lengo baya, lakini sisi hatuna mamlaka kusemea haya, ili kuondoa maneno haya, mamlaka ziharakishe uchunguzi na kutushirikisha hatua muhimu,” alishauri Mruma.

Alisema pamoja na kwamba matukio hayo yameongezeka na kufikia shule tano za Kiislamu kuungua moto katika kipindi kifupi na hakuna ripoti yoyote ya matukio hayo waliopewa na Polisi na mamlaka nyingine za uchunguzi, lakini bado wana imani na vyombo hivyo, ila wanachotamani ni kuharakisha uchunguzi ili wapate majibu ya maswali wanayoulizwa na Waislamu.

“Unajua pamoja na kwamba matukio haya yamehusisha shule zinazosimamiwa na Bakwata, taasisi nyingine za dini yetu na watu binafsi, lakini mwenye dhamana ya kuwasemea Waislamu nchini ni Bakwata, tunaulizwa maswali mengi na hatuna majibu.

“Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) baada ya matukio ya awali aliagiza iundwe Tume ya Uchunguzi, lakini mpaka sasa sisi Bakwata hatuna taarifa yoyote kama iliundwa na ilibaini nini, kwa kuwa maswali ni mengi.

Kwa nini wakati huu?, Kwa nini za Kiislamu, tena baadhi yake ni zile zinazofanya vizuri? Majibu ya haya ni ripoti za mamlaka hata kama sisi tutafanya uchunguzi wetu wa chini kwa chini,” alisema Mruma.

Alisema mpaka sasa wameshapoteza vijana 13 katika matukio ya shule kuungua moto, yakihusisha tukio la usiku wa Septemba 14, mwaka huu katika Shule ya Byamungu Islamic iliyopo wilayani Kyerwa mkoani Kagera iliyosababisha vifo vya wanafunzi 10.

Tukio lingine ni la Shule ya Sekondari ya Ilala Islamic ya jijini Dar es Salaam, ambayo iliungua moto Julai mwaka huu na kusababisha vifo vya wanafunzi watatu.

Shule nyingine za Kiislamu zilizokumbwa na matukio ya kuungua moto lakini bila kusababisha vifo kwa nyakati tofauti mwaka huu ni Kinondoni Muslim na Mivumoni, zote za jijini Dar es Salaam na Kaloleni iliyopo Kilimanjaro; na kufanya idadi ya shule tano.

Shule ya Mivumoni iliungua mara tatu katika kipindi cha miezi miwili, kati ya Julai na Agosti mwaka huu.

Mruma alisema matukio hayo yanaumiza wazazi na Watanzania, kwani licha ya uharibifu mkubwa wa mali, maisha ya watoto waliokuwa na ndoto kubwa yanapotea na kuzimika ghafla.

Alisema taarifa ya uchunguzi ya Polisi wanaisubiri kwa hamu kubwa ili itoe majibu ya kigugumizi cha maswali mengi vichwani mwa watu nchini kote.

Alisema wana imani kubwa na vyombo vya uchunguzi, kwamba vitaharakisha uchunguzi wa tukio la Shule ya Byamungu Islamic na matukio mengine ya nyuma.

Katibu Mkuu huyo wa Bakwata alisema wakati uchunguzi huo ukiendelea, anawashauri wamiliki wa shule zote nchini, za umma, taasisi za dini na binafsi, kuimarisha ulinzi wa ndani wa shule na kuweka miundombinu bora, itakayozuia au kupunguza madhara ya majanga kama hayo mashuleni.

Mruma aliwatoa hofu wazazi wenye watoto katika shule za itikadi hiyo kuwa wawe wavumilivu wakati Bakwata ikishughulikia suala hilo.

Aliwasihi kumuomba Mungu sana ili majanga hayo yasitokee tena na ikiwa kuna uzembe, ujulikane na wahusika wachukuliwe hatua.

Alisema katika shule wanazomiliki wao, mara nyinyi hufanya ukaguzi na kuweka miundombinu mizuri, ila matukio ya moto yamezikumba baadhi ya shule hizo na chanzo chake bado ni kitendawili.

Naye Ofisa Elimu Shule za Msingi Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Ramadhani Marwa ametaja majina ya wanafunzi 10 wa Byamungu Islamic iliyopo kijiji cha Itera, waliokufa wakati moto ulipounguza shule hiyo.

Marwa aliwataja watoto waliokufa kuwa ni Alikani Ally, Samwel Mohamed, Edmundu Erickmass, Abubakari Ibrahim, Oputatus Richald, Alfa Alauni, Abubakary Yasin, Abimari Ibrahim, Adam Silaji na Shadidu Siraji.
 
Alisema watoto wanne kati ya saba waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo, walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, baada ya hali zao kuwa mbaya.
 
Alisema miili ya watoto hao 10 waliokufa kwa kuungua bwenini, iliungua kabisa hivyo ni muhimu kuwatambua kabla ya kuwazika. Alisema miili yao itazikwa baada ya kupimwa vinasaba (DNA) ili kuwatambua.
 
Alisema ratiba ya mazishi itatangazwa baada ya majibu kupatikana. Shule hiyo ina wanafunzi wenye umri kati ya umri miaka 6-13 na wakati ajali inatokea, kulikuwa na wanafunzi 74 bwenini.