Header Ads Widget

JPM 'AMGOMEA' PROF. TIBAIJUKA KUSTAAFU


Prof. Anna Tibaijuka kustaafu
 
 RAIS John Magufuli jana ‘alimgomea’ aliyekuwa mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka uamuzi wake wa kustaafu masuala ya kisiasa.
 
Akiwa wilayani Muleba mkoani Kagera kwa ajili ya kufanya mkutano wa kampeni za kuwania awamu nyingine ya urais, alisema Profesa Tibaijuka bado ana uwezo wa kufanya kazi mbalimbali serikalini.
 
Julai mwaka jana, Profesa Tibaijuka alitangaza kujiweka kando katika masuala ya kisiasa na kueleza kuwa hatogombea tena ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
 
 Profesa Tibaijuka alinukuliwa na vyombo vya habari akitaja sababu ya kung’atuka katika ulingo wa siasa kwamba yeye ni kizazi cha Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliwafundisha kung’atuka.
 
“Mimi mwaka 2020 ninastaafu, ninang’atuka kwa sababu sisi ni kizazi cha Mwalimu Nyerere na katika vitu alivyotufundisha ni kung’atuka.” Alinukuliwa Profesa Tibaijuka.
 
Jana, Rais Magufuli akiwa mkoani hapa alisema kuwa kwake bado hajastaafu masuala ya kisiasa.
 
“Profesa Tibaijuka ameniambia hapa mdogo wangu nimestaafu, mimi nakwambia Profesa haujastaafu, hatuwezi tukamuacha akakaa tu hapa wakati kuna maeneo mengi ya kufanya kazi,” alisema Rais Magufuli.
 
Rais Magufuli alisema, Profesa Tibaijuka ni dada yake na kwamba alipokuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato, mume wake (Profesa Tibaijuka), alikuwa ni balozi Sweden.
 
 “Mama Tibaijuka amesema amestaafu siasa, lakini kwangu mimi hajastaafu, hivyo ni faida ya kuwa na watu sehemu fulani ambao wanaweza kuisaidia serikali. Mimi namwambia kuwa profesa hujastaafu, hatuwezi kumuacha wakati kuna maeneo mengi anaweza kufanya kazi.”