Header Ads Widget

WAZIRI MBARAWA AKAGUA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI MANISPAA YA SHINYANGA




Waziri wa Maji, Prof Makame Mbarawa, akimtwisha ndoo ya maji, mkazi wa kijiji cha Uzogole manispaa ya Shinyanga, Kibibi Elias mara baada ya kuukagua mradi wa maji kijijini hapo.

Na Marco Maduhu -Shinyanga

Waziri wa Maji, Professa Makame Mbarawa leo Agosti 12, 2020 amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika Manispaa ya Shinyanga, ambayo inatekelezwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) pamoja na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA).

Profesa Mbarawa amefanya ukaguzi huo katika miradi ya maji iliyoko Kijiji cha Uzogole, Galamba na Mwawaza-Neghezi, ambayo imekamilika kwa asilimia kubwa pamoja na mengine kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ukaguzi na baada ya kujionea miradi hiyo, Waziri Mbarawa amewataka wananchi kuitunza miundombinu ya maji ili idumu kwa muda mrefu na kuondokana na adha ya kutotumia tena maji ambayo siyo salama kwa afya zao, pamoja na kupoteza muda wa kufuata maji umbali mrefu huku wakikumbana na changamoto ya wanyama aina ya fisi.

“Naombeni sana wananchi wa Shinyanga muitunze miundombinu ya miradi hii ya maji, ili udumu kwa muda mrefu kuwapatia huduma ya maji safi na salama na muondokane na adha ya kutafuta maji umbari mrefu pamoja na kutumia maji ambayo siyo salama,” amesema Mbarawa.

“Maeneo ambayo kuna mradi na hamjapata maji tutaongeza vituo vya kuchotea maji (BP), ili wote mnufaike na maji safi na salama, lengo la Serikali ni kumaliza kabisa tatizo la maji hapa nchini,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, amezitaka mamlaka za maji na wakala wa maji (Ruwasa), kuacha kutumia Wakandarasi kwenye utekelezaji wa miradi ya maji ambayo wana uwezo nayo, bali watumie wataalam wa ndani, (Force Akaunti), ili kupunguza gharama pamoja na miradi hiyo kukamilika kwa wakati.

 Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Shinyanga, Kaimu Meneja Wakala wa Maji Mjini na Vijijini (RUWASA), Julieth Payovela,  amesema miradi ambayo inatekelezwa na mamlaka za maji na Ruwasa imekamilika kwa asilimia kubwa tofauti na ile ya wakandarasi.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, amemuomba waziri huyo wa maji, kuongeza nguvu ya ukamilishwaji wa miradi mikubwa ya maji ambayo ipo Masengwa na Mwakitolyo, ili ikamilike haraka na kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Akielezea utekelezaji wa ujenzi wa tanki kubwa la maji katika mradi wa Mwawaza-Neghezi, Meneja Ufundi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola amesema mradi huo ambao ulianza kujengwa Januari mwaka huu umekamilika kwa asilimia kubwa na kilichobaki ni ujenzi wa chemba na vituo vya maji, na tayari mradi huo wa Sh Bilioni 1 umetumia gharama ya Sh Milioni 900, huku ukitarajia kuokoa takribani Sh Milioni 800 kutokana na kuaminiwa kwa wataalam wa ndani ya mamlaka hiyo.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto walioko mbele) na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (kushoto aliyevaa kofia) wakiwa kwenye ziara kukagua miradi ya maji katika manispaa ya Shinyanga inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA) pamoja na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini wilaya ya Shinyanga (RUWASA) leo Agosti 12, 2020.

Waziri wa Maji, Prof Makame Mbarawa akizungumza mara baada ya kumaliza kukagua miradi ya maji.


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maji.

Kaimu Meneja Wakala wa Maji safi na usafi wa Mazingira Vijijini wilaya ya Shinyanga (RUWASA), Mhandisi Emael Nkopi (Kulia), akielezea utekelezaji wa mradi wa maji katika kijiji cha Galamba manispaa ya Shinyanga.

Mkazi wa Kijiji cha Galamba, Neema Richard, akieleza kufurahishwa na mradi wa maji kijijini kwao ambao utawaondolea changamoto ya maji

Waziri wa Maji, Prof Makame Mbarawa, akinawa mikono kwenye mradi wa maji Galamba.

Kabla ya kuanza ziara yake, Waziri Profesa Makame Mbarawa, aliipokea taarifa ya mkoa wa Shinyanga juu ya utekelezaji wa miradi ya maji.

Kaimu Wakala wa Maji Vijijini Mkoa wa Shinyanga (Ruwasa) Julieth Payovela, akisoma taarifa ya mkoa juu ya utekelezaji wa miradi ya maji.

Waziri wa Maji, Prof Makame Mbarawa (kushoto), akisalimiana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Masovela (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko alipowasili katika ofisi za mkoa huo.

Waziri wa Maji, Prof Makame Mbarawa, akiwasili kwenye ofisi za mkuu wa mkoa wa Shinyanga, kwa ajili ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji.


Picha zote na Marco Maduhu