Header Ads Widget

WATATU WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA UGAIDI
JAMHURI imewafikisha mahakamani watu watatu kwa tuhuma za kuongoza genge la uhalifu, kupanga mikakati ya kigaidi na kutumia sare za jeshi isivyo halali.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili Serikali Mkuu Shedrack Kimaro, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon na Wakili wa Serikali mwandamizi Tulimanywa Majigo huku washtakiwa wakiwa hawana Wakili wa kuwatetea.

Wankyo aliwataja washtakiwa kuwa ni Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya.

Wakili Wankyo alidai katika shtaka la kwanza la kuongoza genge la uhalifu, washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Mei Mosi na Agosti Mosi 2020 katika hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro na katika maeneo mengne ya Dar es Salaam, Morogoro na Arusha kwa pamoja na wengine ambao hawakuwepo mahakamani kwa makusudi alitengeneza mpango wa kutengeneza mikakati ya kigaidi ambayo ni kufanya milipuko katika vituo vya mafuta na mikutano ya hadhara kwa lengo la kuharibu misingi ya kisiasa, katiba, uchumi na sifa ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania

Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa tarehe na maeneo tajwa hapo juu washtakiwa hao kwa pamoja na wengine ambao hawakuwepo Mahakamani walishiriki vikao vya mikakati huku wakijua vina muunganiko wa matukio ya ugaidi ambayo ni kufanya milipuko katika vituo mbali mbali vya mafuta na mikutano ya madhara kwa lengo la kuharibu misingi ya kisiasa, katiba, uchumi na sifa ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania.

Aliendelea kudai kuwa shtaka la tatu linamkabili mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa ambaye anadaiwa Agosti 5, 2020 Katika eneo la Rau Madukani, wilayani Moshi mkoa wa Kilimanjaro alikutwa na dawa za kulevya aina ya Herione zenye uzito wa gramu 3.18, shtaka ambalo pia linamkabili mshtakiwa Lingwenya anayedaiwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa gramu 1.06.

Katika shtaka la tano mshtakiwa Kasekwa anadaiwa Agosti 5, 2020 katika eneo la Rau Madukani alikutwa na silaha aina ya pistol yenye namba A 5340 aina ya Luger bila ya kuwa na kibali Cha umiliki na katika shtaka la Kasekwa anadaiwa kukutwa na vilipuzi ambavyo ni risasi tatu bila ya kuwa na leseni ya umiliki

Katika shtaka la saba mshtakiwa Hassan anadaiwa Agosti 10, 2020 katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuhatarisha usalama wa nchi alitumia sare za jeshi la wananchi JWTZ na Jeshi la kujenga Taifa JKT.

Sare hizo zilkuwa ni suruali moja ya JKT, suruali nne, fulana moja, Koti la mvua moja, jacket moja, kofia tano, overall tano, begi la kubebea vifaa vya lijulikanalo kwa jina la ponjoo, vyeo vinne vya koplo, mikanda minne, soksi pea moja, sweta, beji ya mafunzo ya parachuti, kibuyu cha kunywea maji vyote vikiwa ninmali ya JWTZ pamoja na kisu aina ya AK 47 CCCP.

Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Wakili Kimaro alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Kesi hiyo itatajwa Septemba 2, 2020 na washtakiwa walirudishwa mahabusu.