Header Ads Widget

WALIOKATWA CCM WATOA YA MOYONI,MAKONDA,CHENGE,KITWANGA NA WENGINESIKU moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza majina ya wanachama wake walioteuliwa kupeperusha bendera kwenye kinyang’anyiro cha ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, vigogo waliokatwa wametoa ya moyoni kuhusu uamuzi uliofanywa dhidi yao.

Wakizungumza katika mahojiano maalum na Gazeti la Nipashe, baadhi ya wanachama hao ambao wengine walikuwa mawaziri na wabunge wazoefu, wamesema wamekubaliana na uamuzi uliofanywa na vikao vya juu vya chama.

ANDREW CHENGE

Aliyekuwa Mbunge wa Bariadi mkoani Simiyu, Andrew Chenge, ambaye ameongoza kura za maoni katika jimbo hilo, alipoulizwa kuhusu uamuzi uliofanywa dhidi yake, alijibu kwa kifupi kwamba amefurahi sana.

Nimefurahi sana,” alijibu Chenge ambaye amekuwa mbunge kwa kipindi kirefu na kutoa mchango mkubwa katika utungaji wa sheria na uandaaji wa bajeti ya serikali.
Nipashe pia iliuliza Chenge kama yuko tayari kushiriki kampeni kukisaidia chama kupata ushindi na akatoa jibu lilelile kwamba amefurahi sana.

DK. HARRISON MWAKYEMBE

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye ameanguka katika kumsaka mgombea wa CCM Jimbo la Kyela mkoani Mbeya, amesema ameupokea uamuzi wa vikao vya juu vya chama kwa mikono miwili na atashirikiana na wateule kukiwezesha chama kupata ushindi.

Ninayaheshimu maamuzi ya chama. Kilichobaki ni kukisaidia ili wateule waweze kupata ushindi," alisema Dk. Mwakyembe ambaye katika kura za maoni alishika nafasi ya tatu.

ADADI RAJABU

Aliyekuwa Mbunge wa Muheza mkoani Tanga, Adadi Rajabu, pia amesema ameupokea kwa 'roho moja tu' uamuzi wa vikao vya juu vya CCM na kuahidi kushiriki kumpigia kampeni mgombea aliyepitishwa na chama hicho kuwania ubunge wa jimbo hilo.

“Maamuzi ya vikao nimeyapokea kwa roho moja tu na tutaendelea kumpigia debe kampeni zitakapoanza Mwana FA ambaye ameteuliwa. Haya ni maamuzi ya chama ambayo yanataka kukijenga chama,” amesema Mkurugenzi huyo wa zamani wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

PAUL MAKONDA

Amesema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, pia ametumia  ukurasa wake rasmi wa Instagram kutoa maoni yake kuhusu uteuzi huo akisema.

"Ninamwabudu Mungu aliye hai, hata kama asipojibu sawa na maombi yangu, bado atabaki kuwa Mungu wangu."

Makonda amelazimika kupoteza cheo  cha ukuu wa mkoa alipochukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM kuwania ubunge wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambako alishika nafasi ya pili kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho nyuma ya kinara Dk. Faustine Ndugulile ambaye pia ameteuliwa na vikao vya juu vya chama.

CHARLES KITWANGA

Aliyekuwa Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga, amesema aliyeteuliwa na chama ni uamuzi wa Mungu na hivyo hana sababu ya kupinga uamuzi uliotolewa na vikao vya juu vya chama.


“Ninampenda mwenyezi Mungu, ninampenda Rais wangu, ninakipenda chama changu.
Nitashiriki kampeni kama kawaida, mimi ni mtu wa Mungu, siwezi kumkosea Mungu, akitoka Mungu juu duniani, anakuja Rais, hakuna mwingine. Sasa kama ninampenda Mungu, nitashindwaje kumpenda Rais?” alihoji.

Kitwanga 

amesema Rais John Magufuli ni rafiki yake wa siku nyingi, hivyo anaamini kila anachokifanya ni kwa nia njema na yeyote atakayezungumza kinyume chake, atakuwa anamkosea Mungu.

“Huyu ndugu yangu (Rais Magufuli) amefanya mambo mengi, mimi nimetembea nchi hii kila sehemu, nimepita wakati pakiwa pabaya, nimepita wakati pakiwa pazuri, amefanya vizuri siyo tu kwenye nchi bali hata kimataifa, maisha yangu ni Tanzania yangu,” amesema.

VENANCE MWAMOTO

Aliyekuwa Mbunge wa Kilolo mkoani Iringa, Vanace Mwamoto, amesema amefurahishwa na uteuzi huo na kazi yake kubwa iliyopo mbele yake ni kuhakikisha chama kinashinda.

Mimi ni mwanachama wa CCM, ninaamini inapotokea mchakato kama huu, kuna mmoja lazima apeperushe bendera, mwingine anabaki. Kwa hiyo, mimi sasa hivi hapa ni kuhakikisha chama changu kinashinda kwa sababu mwisho wa siku na mimi nilimtoa mtu," amesema.

MARY CHATANDA

Mary Chatanda, aliyekuwa Mbunge wa Korogwe Mjini mkoani Tanga, amesema amepokea vizuri uamuzi wa chama kwa sababu ni utaratibu wa chama kila inapotokea kipindi cha uchaguzi, wanachama wanajitokeza wengi kugombea na mwisho anateuliwa mmoja.

“Mimi pamoja na kwamba niliongoza kwa kura, lakini bado chama kimekukaa vikao vyake na kumteua mwanachama mwingine ili kupeperusha bendera katika jimbo la Korogwe. Mimi sina shaka kabisa, nimeukubali, nimeupokea,” amesema.

Source IPP Media