Header Ads Widget

TUTAHAKIKISHA AMANI INADUMU WAKATI WOTE IGP SIRRO


Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro (pichani) amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu, polisi wamejipanga kuhakikisha amani inadumu.
Amewataka viongozi wa vyama vya siasa, kutumia majukwaa katika mikutano ya hadhara kuhubiri amani na utulivu. amesema hayo wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa na makamanda wa Jeshi la Polisi makao makuu ya jeshi, mjini hapa.
Sirro amesema jeshi la polisi halitamvumilia kiongozi wa chama cha siasa, atakayejaribu kuhatarisha amani kwa kutumia kisingizio cha mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa.
“Harakati za uchaguzi mkuu tayari zimepamba moto na polisi wamekabidhiwa majukumu ya kulinda amani na utulivu, hivyo wanasiasa tunawaomba waitumie mikutano ya kampeni kuhubiri amani na utulivu,” amesema.
Amesema watanzania wanahitaji utulivu wa kisiasa, kwani baada ya uchaguzi mkuu maisha yanatakiwa yaendelee kama kawaida, kwa ajili ya kuleta maendeleo na kuimarisha uchumi wa wananchi.
Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mohamed Haji Hassan amesema lengo la kikao hicho ni kubadilisha mawazo na kujenga mikakati madhubuti, ambayo itawafanya wanasiasa kufanya shughuli za kampeni ikiwemo mikutano yao kwa kupata ulinzi kutoka jeshi la polisi.
“Hiki ni kikao muhimu ambacho kinajenga mahusiano mazuri kati ya viongozi wa polisi na wanasiasa na hatimaye kuona wanafanya mikutano ya kampeni katika mazingira ya amani na utulivu,” amesema.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi anayeshughulikia Polisi Jamii, Dk Mussa Ali Mussa amesema uchaguzi mkuu kwa upande wa Zanzibar, kwa kawaida hukabiliwa na changamoto nyingi ikilinganishwa na Tanzania Bara, kutokana na ukweli kwamba Zanzibar upo utashi mkubwa wa kisiasa
. “Nilipata kuwa Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa upande wa Zanzibar nayafahamu vizuri mazingira ya kisiasa hasa unapofika wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu, joto la kisiasa hupanda juu...huu ni wakati wa kufanya uchaguzi huru usiokuwa na jazba za kisiasa ili tulinde uchumi wetu na ustawi wa jamii,” amesema.

Source Habarileo