Header Ads Widget

RAIS WA UTPC AITEMBELEA KLABU YA WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA



Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratias Nsokolo akizungumza na wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Shinyanga (SPC), leo Agosti 25, 2020 mjini Shinyanga.

Na Damian Masyenene -Shinyanga
LEO Agosti 25, 2020 Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo ameitembelea Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania (SPC) na kufanya mazungumzo na viongozi na wanachama wa klabu hiyo, huku akitoa wito kuhakikisha wanaongeza wanachama wapya kwani bado idadi kubwa ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga bado hawajajiunga na klabu hiyo.

Nsokolo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Kigoma na Mwandishi wa habari mkongwe, ameipongeza SPC kwa kufanikisha uchaguzi wake mkuu kwa amani na kupata viongozi wapya, huku pia akimsifu Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Kadama Malunde kwa uongozi wake wa miaka mitano uliotukuka.



Hadi sasa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (SPC) inao wanachama 39, huku mkoa huo ukiwa na waandishi wa habari 97, ambapo Nsokolo amewahimiza waandishi kujiunga na klabu ili kuwa wamoja na kuwa na sauti ya pamoja yenye nguvu.

Mbali na hilo, Nsokolo pia amewashauri wanachama hao wa SPC kujiunga na bima ya afya na kuwataka waandishi wa habari kuona umuhimu wa huduma hiyo kwa sababu katika uhalisia maisha ya uandishi wa habari Tanzania yanafahamika kwani hakuna mishahara ya uhakika, mikataba wala kipato kinachoeleweka.

"Mara nyingi tukipata matatizo ni ya kwetu na familia zetu, watu waelimishwe waone haja ya kujiunga na bima, tutoe umuhimu kwenye mambo ya msingi yanayohusu maisha yetu na familia zetu....kwahiyo nategemea waandishi wa habari Tanzania tuanze kujitengenezea utaratibu wa kulinda afya zetu," amesema.

Akizungumzia umuhimu wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Nsokolo amesema imekuwa na msaada mkubwa kwa waandishi wa habari kwa kufanikisha mambo mbalimbali ikiwemo kugharamikia ofisi zao, uendeshaji, mafunzo na motisha mbalimbali, hivyo akasisitiza iendelee kuungwa mkono na changamoto zilizopo zitafanyiwa kazi.
Licha ya mafanikio hayo, Nsokolo ameonya waandishi wa habari kutozingatia weledi katika majukumu yao na kuigeuza UTPC kama kichaka cha kuficha makosa yao ya jinai, hivyo hawako pale kuyatetea maovu hayo.
"Tufuate misingi yetu kwenye uandishi na tuzingatie maadili tusijikute kwenye matatizo, tusichoke kutengeneza mahusiano na wadau na pale panapolega tuparekebishe," amesema.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Shinyanga (SPC), Patrick Mabula ametoa wito kwa wanachama wake kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, huku akiwahimiza kuwasilisha kwa maandishi changamoto na malalamiko ya mambo mbalimbali yanayokiukwa ili yaweze kushughulikiwa.
Mwanachama wa SPC, Moshi Ndugulile ameiomba UTPC kulitafutia ufumbuzi suala la waandishi wa habari nchini kutokuwa na dhamana ya kupata mikopo kwenye taasisi mbalimbali za kifedha, ambao aliwasihi walipiganie suala hilo lipate ufumbuzi.

 Rais wa UTPC, Deogratias Nsokolo akiendelea na mazungumzo na wanachama wa SPC