Header Ads Widget

CHF ILIYOBORESHWA MANISPAA YA SHINYANGA YAANDIKISHA KAYA 1,832, KUZIFUFUA ZINGINE 6,302



Mratibu wa CHF Iliyoboreshwa Manispaa ya Shinyanga, Jackson Njau

 Na Damian Masyenene –Shinyanga
Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF iliyoboreshwa) katika Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga imeandikisha jumla ya Kaya mpya 1,832 kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Juni 2020, ambapo imeweka mkakati wa kuzifufua kaya zingine 6,302 ambazo zimemaliza muda wake (expire), huku wakilenga kuzifikia mpya zaidi ya 20,000.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa CHF iliyoboreshwa Manispaa ya Shinyanga, Jackson Njau wakati akizungumza na Shinyanga Press Club Blog ofisini kwake jana, ambapo alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo katika manispaa yake jumla ya kaya 16,320 zimeandikishwa hadi sasa.
 Jackson Njau akizungumza jana ofisini kwake

Mratibu huyo alieleza kuwa kwa sasa kaya zilizo hai zinazopata huduma hiyo ni sawa na asilimia 7.3, ambapo wanalenga kufikia asilimia 20 kufikia Juni 2021 ikiwemo kuzifufua kaya zingine 6,302 ambazo muda wake umeishia.

“Mkakati ni kuhakikisha tunatengeneza ushirikiano na waratibu wa afya katika maeneo yao na Kamati za afya ngazi ya jamii ambao watahamasisha na wao kuwa mfano, kwa sasa huduma zimeboreshwa katika manispaa yetu.

“Tumejipanga kuanzia ngazi ya mtaa mpaka halmashauri kupitia maafisa uandikishaji kuwakumbusha wanachama kuhuisha taarifa na huduma zao kwa kuwatembelea na kupitia namba zao za simu,” alisema.

Njau pia alieleza kuwa kwa sasa mwitikio wa wananchi kujiunga na huduma hiyo unaridhisha kutokana na elimu ya uhamasishaji waliyoifanya, ambapo sasa mkakati ni kushirikiana na timu ya mkoa kuanza uhamasishaji katika kata zote 17, mitaa na vijiji 72 vya manispaa hiyo.

Pia kukaa na maofisa maendeleo ya jamii, watendaji kata na vijiji kufanya uhamasishaji kuongeza kaya kwenye mpango huo, pia wakuu wa idara nao kuhamasisha huduma hiyo katika sekta mbalimbali.

Mmoja wa wakazi wa Manispaa ya Shinyanga, Joachim Kuyela (80) kutoka Kata ya Masekelo ambaye alifika ofisini hapo kujiunga na huduma hiyo akiambatana na familia yake, alieleza kuwa sababu kubwa iliyomsukuma kwenda CHF iliyoboreshwa ni kutokana na kusongwa na matatizo mengi ya kiafya huku uwezo wa kipato ukiendelea kupunguza.

“Hali ya maisha yangu nimezeeka siyo wakati wote naweza kuhudumia familia kutoa fedha za matibabu, nilikuwa natumia gharama kubwa kwahiyo tumeona tuje tupate bima,” alisema.