Header Ads Widget

KATAMBI: NIMEZUNGUMZA NA MASELE KUOMBA BARAKA ZAKE, AMEFURAHI

Patrobasi Katambi akiwapungia mkono wananchi wakati akipita katika mitaa ya Manispaa ya Shinyanga leo Jumamosi baada ya kuchukua fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini. Picha na Kadama Malunde

Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog 
Mgombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrobasi Katambi leo Agosti 22, 2020 amechukua fomu ya kugombea rasmi nafasi hiyo katika ofisi ya Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, huku akiwahakikishia wanachama kuwa kila kitu kiko sawa baada ya kupata ushirikiano kutoka kwa mbunge anayemaliza muda wake, Steven Masele. 

Katambi ametoa kauli hiyo leo katika ofisi za CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini alipokuwa akizungumza na wanachama, wagombea udiwani katika kata 17 za jimbo hilo na baadhi ya makada waliotia nia ya ubunge. 

Katambi alipitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuwa mgombea wa chama hicho licha ya kushika nafasi ya saba kwa kupata kura 12, huku Mbunge anayemaliza muda wake, Masele akishinda katika mchakato wa kura za maoni baada ya kupata kura 152. 

“Waliokuwa wagombea wenzangu wote 59 wameniahidi ushirikiano, nimezungumza leo asubuhi na Masele anawapa salamu nyingi na amewashukuru kwa muda wote aliokuwa nanyi, ameahidi kuendelea kutusaidia na kutuunga mkono kwa mambo mbalimbali yenye maslahi na jimbo letu,” alisema Katambi. 

Awali Agosti 20, 2020 baada ya Katambi kutangazwa kuwa mgombea rasmi wa ubunge jimbo la Shinyanga Mjini, Masele kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter aliandika "Nimepokea kwa heshima kubwa maamuzi ya chama changu.Nawashukuru wananchi wa jimbo la shinyanga mjini,viongozi wote wa chama changu ngazi zote kwa kunipa fursa ya kuwa mbunge kwa miaka kumi.Tushikamane kukipigania chama kiweze kushinda uchaguzi mkuu.Binafsi nitashiriki kikamilifu"

Katika zoezi la uchukuaji fomu na kuwashukuru wanachama, Katambi amesindikizwa pia na baadhi ya makada wa CCM waliotia nia ya ubunge na miongoni mwao waliopata nafasi ya kuzungumza ni Jonathan Manyama aliyeshika nafasi ya pili kwenye mchakato wa kura za maoni nyuma ya Steven Masele, mwingine aliyezungumza ni Bandora Milambo ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa umoja wa watia nia wa CCM jimbo la Shinyanga Mjini. 

Manyama amewatahadharisha baadhi ya watu watakaojaribu kupingana na chama kwa maamuzi yake ya kumpitisha Katambi kuwa mgombea ubunge wa Shinyanga Mjini. 

“Tunautangazia umma kwamba mgombea wetu ni mmoja nan i Katambi, na wote kwa pamoja tulikubaliana kumuunga mkono bila kujali ushindani tuliokuwa nao, mtu asijaribu kupingana na CCM kwa kumpitisha Katambi, atajikuta matatizoni,” amesema. 

Naye Milambo amesema watia nia wote wa ubunge jimbo la Shinyanga Mjini wamekubali kuungana na kutengeneza umoja ili kukisaidia chama kushinda bila kujali ni nani kati yao aliyepitishwa.