Header Ads Widget

NKULILA, GULAM, MWENDAPOLE WAPETA KWA KISHINDO, VICTOR MKWIZU ASHINDA NGOKOLO



Hafidh Mukadam Gulam

LEO zoezi la upigaji kura za maoni kwa watia nia wa nafasi za ubunge wa kata ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) limeendelea katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo katika mkoa wa Shinyanga aliyekuwa Mstahiki Meya wa manispaa ya Shinyanga, Gulam Hafiz Mukadam  ameshida kura za maoni kata ya Mjini.
Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Julai 25,2020 Gulam alikuwa anatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Miti Mirefu, Nassoro Warioba lakini hali ikawa tofauti na kuibuka kidedea.
Gulam amepata kura 25 kati ya 42, huku Nassoro akiambulia kura 4.

Mshike mshike mwingine ulikuwa  Kata ya Ndembezi ambapo aliyekuwa Diwani David Nkulila ameshinda kwa 54 dhidi ya 33 za Victor Thobias Manywa, huku Winsslaus Maganga akiambulia kura moja na Robert Mwelo akikosa kura, ambapo wapiga kura walikuwa ni 88.

Katika Kata ya Ngokolo ambayo CCM wanahitaji kuirejesha kutoka mikononi mwa upinzani,wapiga kura walikuwa 74, ambapo Victor Mkwizu ameibuka mshindi kwa kupata kura 19.

 Victor Mkwizu 'Sangu'
Hata hivyo, Mkwizu alipata ushindani mkubwa akibebwa na kura moja tu mbele ya mpinzani wake, Cecilia Shangaluka aliyepata kura 18, huku Fravel Makwaya na Fue Mlindoko wakipata kura 13 kila mmoja.

Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo, Rebeka Magoma ambaye ni Katibu wa UWT mkoa wa Shinyanga amewataka wagombea hao kudumisha amani kipindi hiki wakisubiri uamuzi wa mwisho wa chama.

"Nina imani mtashirikiana hamtampinga mtu kwani tunahitaji kuuondoa uyatima tuwe kitu kimoja," amesema Magoma.

Akiwashukuru wajumbe wa mkutano huo, Victor Mkwizu amewaomba ushirikiano wanachama wenzake katika kuipeperusha bendera ya CCM.

 Wajumbe wa uchaguzi huo kutoka Kata ya Ngokolo
Kata ya Kambarage, aliyekuwa diwani, Hassan Mwendapole ameibuka kidedea akipata ushindi wa kishindo mbele ya washindani wake baada ya kukusanya kura 46 kati ya 79 zilizopigwa, huku mshindani wake wa karibu Emmanuel Kidinya akipata kura 13, Rehema Namanyiro kura 7, Majjid Issa kura 7 na Joyce Masunga kura 4.