Header Ads Widget

MWIGIZAJI MWIJAKU AFIKISHWA MAHAKAMANI, ASHINDWA KUPATA DHAMANA


 
MSANII wa uigizaji nchini, Mwemba Burton (35) maarufu kama Mwijaku amepandishwa kizimbani cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kusambaza picha za utupu (ngono).

Msanii huyo ambaye hivi karibuni alijitosa kwenye siasa na kutia nia ya kugombea ubunge jimbo la Kawe amesomewa mashtaka yake leo Julai 29 2020, na Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon akisaidiwa na wakili wa serikali Mwanamina Kombakono mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.

Akisoma hati ya mashtaka wakili Kombakono amedai kuwa kati ya tarehe 17 Septemba 2019 na tarehe 10 Oktoba 2019, mshtakiwa Mwijaku kwa kutumia mtandao wa Whatsapp alisambaza picha za utupu mtandaoni.

Hata hivyo, mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo amekana na amerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Hakimu Kabate amesema mshtakiwa ana heshima zake kwenye jamii kwa kuwa anaheshima zake anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye heshima zao na wengine wawili, mmoja kati yao anatakiwa atoke sehemu moja wapo aidha Bongo movie au Tasnia ya Muziki.

Pia mahakama imeamuru barua zao lazima ziwe na baraka za Baraza la sanaa Basata huku kila mmoja akitakiwa kusaini bondi ya sh. Laki tano.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, sehemu kubwa ya upelelezi katika shauri hilo umekamilika imebakia sehemu ndogo hivyo wameomba ipangiwe tarehe nyingine.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 12 Agosti 2020 itakapokuja kwa kutajwa. ambapo hadi shauri hilo linaahirishwa Mwijaku alikuwa hajafanikiwa kutimiza masharti ya dhamana.