Header Ads Widget

AKINA MAMA KAHAMA WASISITIZWA KUWANYONYESHA WATOTO KWA MIEZI SITA MFULULIZO

 
  Akina mama wenye watoto chini ya miezi sita wa Kata ya Majengo halmashauri ya mji wa Kahama wakiwa katika semina ya kupewa elimu kuhusu unyonyeshaji wa watoto. 
Na  Patrick Mabula- Kahama
Akinamama wajawazito wanapojifungua wametakiwa kufuata elimu ya watalaam wa afya kuhusu kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama kwa miezi sita mfululizo bila kumpatia rishe yoyote hali inayomfanya mtoto kuwa na afya bora ya mwili na akili.

Wito huo umetolewa mjini Kahama na Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto wa Halmashauri ya mji wa Kahama, Carolyne Marcel katika tamasha la kutoa elimu kwa akina mama wanaonyonyesha watoto walio chini ya miezi sita, lililoandaliwa na SHDEPHA+ katika mradi wake wa TULONGE AFYA kwa lengo la kuwafundisha  unyonyeshaji bora.

Marcel alisema mama anapojifungua anapaswa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwa miezi sita mfululizo na hatakiwi  kumpatia rishe ya aina yoyote kwa kipindi hicho, ili kumsaidia mtoto kukua  vizuri kwa afya bora na akili yenye uelewa mpana  atakapokuwa mkubwa kwa sababu maziwa ya mama  yana virutubisho muhimu.

Naye Mratibu wa Huduma ya afya ya jamii na elimu kwa umma wa halmashauri ya mji wa Kahama, Asteria Kamanga  amewataka akina mama kufuata elimu wanayopewa na watalaam wa afya kuhusu malezi bora ya watoto katika kuwanyonyesha maziwa ya mama wanapojifungua  kwa sababu yanawasaidia watoto kukua vyema kimwili na kiakili.

Kwa upande wao baadhi ya akina mama waliohudhuria hafla hiyo, wenye watoto chini ya miezi sita wanaonyonyesha waliwataka  wenzao kuachana na elimu ya mitaani inayopotosha katika malezi ya mtoto, bali wazingatie elimu ya wataalam wa afya ili kuhakikisha mtoto anakuwa vizuri.

Meneja mradi wa Tulonge Afya unaotekelezwa katika halmashauri ya mji wa Kahama na Shirika la SHDEPHA+, Martin Kitina  amesema lengo ni  kutoa elimu kwa akina mama wanaojifungua namna ya unyonyeshaji mzuri kwa mtoto kwa miezi sita mfululizo.

Meneja Mradi wa Tulonge Afya wa Shirika la SHDEPHA+, Martin Kitina akizungumza katika hafla ya utoaji elimu kwa  akina mama wanaonyonyesha watoto walio chini ya miezi sita wa Kata ta Majengo wilayani Kahama kuhusu unyonyeshaji bora wa mtoto maziwa ya mama kwa miezi sita.


 Mratibu wa Mradi wa Tulonge Afya wa Shirika  TMARC Tanzania mkoa wa Shinyanga, Mgalula Ginai akiwaasa akina mama wa Kata ya Majengo mjini Kahama kuzingatia elimu ya wataalam wa afya juu ya unyonyeshaji wa watoto kwa miezi sita mfululizo.


Mratibu wa huduma ya afya ya jamii elimu kwa umma wa halmashauri ya mji wa Kahama, Asteria Kamanga alipokuwa akitoa mada katika hafla hiyo katika utekelezaji wa mradi wa Tulonge Afya unaosimamiwa na SHDEPHA+.
 
Baadhi ya akina mama hao wakifuatilia ushauri uliotolewa na wataalam wa afya kutoka shirika la Shidepha+
 
Washiriki wa hafla hiyo wakiwa katika picha ya pamoja
Picha zote na Patrick Mabula