Header Ads Widget

MGOGORO BAINA YA WENYEVITI WA KIJIJI NA KITONGOJI MISSENYI WADAIWA KUKWAMISHA MAENDELEO


Wananchi wa Kijiji cha Omudongo wilayani Missenyi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara

Na Avitus Mutayoba-Missenyi
Wananchi katika kijiji cha Omundongo kata ya Kassambya wilayani Missenyi Mkoa wa Kagera wamedai kijiji hicho kinashindwa kutekeleza shughuli za maendeleo kutokana na mgogoro baina ya mwenyekiti wa kijiji na mwenyekiti wa kitongoji cha Omukitwe ndani ya kijiji hicho.

Katika mkutano wa hadhara uliolenga kujadili shughuli za maendeleo ndani ya kijiji, baadhi ya wananchi akiwemo Johanes Patrick, Gelda Mushashu pamoja na Abbas Rweyendela walisema kuwa mgogoro huo umedumu kwa zaidi ya miezi sita kwa viongozi hao kushindwa kufanya kazi kwa pamoja.

Wameongeza kuwa hali hiyo inapelekea kushindwa kusimamia ulinzi na usalama wa kijiji na kusababisha vitendo vya wizi kushamiri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho, Anastazius Tushabe amesema kuwa chanzo cha mgogoro huo ni mwenyekiti wa kitongoji cha Omukitwe, Hamad Mwinyi kukataa kuunda vikosi vya ulinzi shirikishi licha ya kuripotiwa wizi wa mara kwa mara.

Na hata alipopewa nafasi ya kujitetea mbele ya mkutano, Hamad Mwinyi ameeleza kuwa hoja hiyo haina ukweli ndani yake na badala yake mwenyekiti wa kijiji amekuwa akitengeneza njama za kudhoofisha uongozi wake.

Kwa mujibu wa  Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Omundongo, Rashid Yusuph amesema kuwa viongozi hao wanaotokana na chama hicho wameshasuluhishwa zaidi ya mara tatu na kuahidi kumaliza mgogoro huo bila mafanikio hivyo chama kinakusudia kuwachukulia hatua.

Aidha, Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Edjest Kaijage amekiri vikao vya usuluhishi kuwaita na kuwasuluhisha mara tatu bila mafanikio na kuongeza kuwa taarifa za mgogoro huo zipo katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri.

Hata hiyo mwandishi wetu anazidi kufuatilia katika ofisi za mkurugenzi wa halmashauri ili kujiridhisha juu ya hatua zinazokusudiwa kuchukuliwa ili kumaliza mgogoro huo.

Mwenyekiti wa kijiji, Anastazius Tushabe akiendesha mkutano

Wananchi wakifuatilia mkutano