Header Ads Widget

MBARONI KWA KUKODISHA BUNDUKI MAJAMBAZI























POLISI mkoani Tabora imemkamata Ramadhan Juma (65) mkulima, mkazi wa Kijiji cha Ndekela, Kata ya Tongi, Tarafa ya Puge wilayani Nzega, kwa tuhuma za kukodisha silaha, shotgun kwa majambazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Barnabas Mwakalukwa alisema silaha hiyo yenye namba za usajili TZCAR 36462 na risasi zake nne, ilikamatwa Juni 19, mwaka huu saa 11.30 za jioni ikiwa imehifadhiwa katika nyumba ya mtuhumiwa huyo.

Kamanda Mwakalukwa alisema silaha hiyo alikuwa akiikodisha kwa wahalifu waliokuwa wakiitumia katika matukio ya wizi na unyang’anyi.

Alisema baada ya msako wa kina, pia walimkamata Athuman Salum (30), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Ndekeli na wenzake watatu ambao wamekuwa wakijihusisha na matukio ya ujambazi kijijini hapo.

Kamanda Mwakalukwa alisema baada ya kupekuliwa katika makazi yao, watuhumiwa hao walikutwa na vipande vya nondo, visu vinne na mapanga ambavyo hutumika kutekeleza kazi zao za kihalifu.

Aidha, zilipatikana fedha taslimu Sh 500,000 zimefichwa uvunguni mwa kitanda cha mtuhumiwa ambazo zinasadikika ziliporwa kwa wananchi katika tukio la ujambazi lililofanyika hivi karibuni kijijini hapo. Alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea na watuhumiwa wanahojiwa na watafikishwa kortini.