Header Ads Widget

MAKADA 323 WACHUKUA FOMU ZA UBUNGE MKOA WA SHINYANGA Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga, Ernestina Richard akimkabidhi fomu mmoja ya wanachama.
Na Suzy Luhende -Shinyanga
WAKATI zoezi la uchukuaji fomu za kuomba ridhaa ya kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi za ubunge na udiwani likihitimishwa leo Julai 17, 2020 saa 10 jioni, imebainishwa kwamba katika mkoa wa Shinyanga jumla ya Makada 323 wamechukua fomu.
Makada hao ni kutoka majimbo Sita ya mkoa huo ambayo ni Shinyanga Mjini, Kahama Mjini, Solwa, Kishapu, Ushetu na Msalala.
Ambapo idadi hiyo inaonyesha kwamba Jimbo la Shinyanga mjini wagombea ni 60 kati ya hao wanawake ni saba na wote wamerudisha fomu.
 Jimbo la Solwa wamejitokeza wagombea 54, Jimbo la Kishapu wapo 78 ambao wote wamerudisha fomu.

Katika jimbo la Msalala wagombea walikuwa 44 na wamerudisha fomu wote, Jimbo la Ushetu wagombea waliochukua fomu ni 17 wote wamerudisha fomu na Kahama Mjini wagombea walikuwa 70 wote wamerudisha fomu.

Katika Jimbo la Shinyanga mjini wanawake waliojitokeza kuchukua fomu ni saba, Jimbo la Solwa ni wanawake wanne, na Jimbo la Kishapu wamejitokeza kuchukua fomu wanawake wanne.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini, Said Bwanga amesema wanachama wote wamerudisha fomu, ambapo amewataka wananchi kuchagua kiongozi bora na kwamba wapiga kura wasishawishike na chochote.

Naye Katibu Mwenezi wa wilaya ya Shinyanga, Emmanuel Lukada amesema wapiga kura waangalie mtu atakayewafaa kuwatumikia waachane na rushwa.

Baadhi ya wananchi waliozugumzia zoezi hilo akiwemo Yohana Paul na Kabla Richard wamesema wao wanahitaji mbunge atakayewaletea maendeleo na hawatoshawishika kirahisi kwa rushwa.