Header Ads Widget

WATOTO 232 MWANZA WADAIWA KUFANYIWA UKATILI WA KINGONO KWA KIPINDI CHA MIEZI 3




Baadhi ya watoto walioshiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, 2020 jijini Mwanza
Na Mwandishi Wetu - Shinyanga Press Club Blog
Takwimu zinaendelea kuonyesha kuwa bado watoto wako kwenye hatari kubwa ya vitendo vya ukatili hasa watoto wa kike ambao wanakabiliwa na matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Mwanza.
Hilo linathibitishwa katika taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella katika maadhimisho ya siku ya mtoto Afrika duniani kwa mkoa wa Mwanza, iliyowasilishwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt.Severine Lalika Juni 16, 2020, ambapo imeelezwa kuwa jumla ya watoto 232 wametajwa kufanyiwa matukio ya ukatili ya kingono kwa kipindi cha Januari hadi Machi, 2020.

Akiwasilisha taarifa hiyo kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto Afrika duniani kwa mkoa wa Mwanza yaliyofadhiliwa na Shirika la Plan International, Dkt. Lalika amesema kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Polisi mkoani humo kuanzia Januari hadi Machi, 2020 jumla ya matukio 234 yaliripotiwa, kati yao wavulana wakiwa 17 na wasichana 219.

Amesema katika matukio hayo, visa vya mimba za wanafunzi zilikuwa 143, kubakwa 57 na kulawitiwa matukio 17, ambapo amewataka maofisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii mkoani humo pamoja na halmashauri kuimarisha utoaji elimu ya malezi na makuzi ya watoto kwa wazazi na walezi ili wawalee watoto kwa misingi ya haki na usawa wa kijinsia.

"Mwaka 2019 matukio ya kingono yalikuwa 420, wasichana wakiwa 393 na wavulana 37 kati ya hayo mimba za wanafunzi zilikuwa 188, 148 kubaka, 39 kulawiti na 34 yalikuwa ya kufanya mapenzi na wanafunzi," ameeleza Dkt. Lalika.

Meneja wa Shirika la Plan International Tanzania mkoa wa Mwanza, Dk. Majani Rwambali akizungumza na wanahabari

Kwa upande wake Meneja wa kitengo cha watoto kutoka Plan International Tanzania Mkoa wa Mwanza, Dk. Majani Rwambali amesema wametoa elimu na mafunzo ya kuwahamasisha vijana ambayo yameleta hamasa kwa vijana kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili.

Anasema mipango na rasimali zao wamezielekeza katika kumlinda na kumwendeleza mtoto na kutekeleza sheria zote za nchi ili kuweza kufikia malengo mbalimbali yaliyowekwa kwa ajili ya kusaidia na kumwendeleza mtoto, huku mkakati uliopo ni utoaji wa elimu katika sehemu mbalimbali za mkoa wa Mwanza .

"Idadi ya matukio yanaongezeka kwa sababu watoto wanaopata mimba ni wengi, baada ya kutoa elimu jamii imepata uelewa na ujasiri wa kutoa taarifa kwenye vyombo ambapo inawezekana, huko nyuma kulikuwa na matukio mengi zaidi na watu hawakujua wapi pakuyasemea lakini sasa wanatambua haki zao," amesema Rwambali.


Baadhi ya watoto na washiriki waliohudhuria maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika kwa mkoa wa Mwanza

Mwenyekiti wa Baraza la watoto Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Joel Festo ameeleza kuwa vitendo vya ukatili wa kingono wanavyokabiliwa navyo watoto hao huwahathiri kisaikolojia, hali ambayo hutokana na wazazi wengi kutumia muda wao mbali na watoto na kupewa majukumu makubwa ikiwemo kufanya biashara .

Mjumbe wa Baraza la watoto Mwanza, Mariam Daud amebainisha kwamba kwa sasa watoto wa kiume hulawitiwa kutokana na wazazi na jamii kutokuwa na utambuzi wa masuala hayo pamoja na ulinzi 
  
"Mahusiano mabaya na migogoro ya kifamilia wakati mwingine hunachangia watoto kufanya shuguli hatarishi ambazo hupelekea kuwa na ongezeko kubwa la watoto wa waishio mitaani, ndugu kuwafanyia ukatili, walevi na wasiokuwa na maadili hivyo wazazi, walezi na jamii iwalinde watoto na kuwawekea muda maalum wa kutumia vifaa vya kielektroniki," amesema Mariam.


Baadhi ya washiriki wa maadhimisho hayo wakiwa katika picha ya pamoja.