Header Ads Widget

OXFAM YAWAKUMBUKA WATAALAMU WA AFYA MSALALA



Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege (Kushoto) akipokea vifaa kinga kutoka shirika la OXFAM
Na Salvatory Ntandu - Msalala
Katika jitihada za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, Shirika la OXFAM limetoa msaada wa vifaa kinga mbalimbali vya kujikinga na maambukizi kwa wataalamu wa afya vyenye thamani ya Sh Milioni 29.8. 

Vifaa hivyo vimekabidhiwa leo June 17, 2020 na Mratibu wa Miradi wa Shirika la OXFAM Kanda ya Ziwa,Valentine Shibula kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Simon Berege.
  Akikabidhi vifaa hivyo, Shibula amesema wametoa msaada huo kwa lengo la kuunga mkono jitihada za serikali katika mapambano dhidi ya Corona kwani OXFAM inatambua umuhimu wa huduma zinazotolewa na wataalamu wa afya, hivyo imetoa vifaa hivyo ili kuwakinga na maambukizi pale wanapokwa wanawahudumia wagonjwa katika vituo mbalimbali vya afya maalumu vilivyotengwa na serikali.

“Vifaa tulivyowaletea leo ni pamoja na Barakoa za (N95) 240, Mavazi maalumu ya kujikinga na Corona (PPE), Jezi 60, vidonge vya kutakasa vifaa tiba vinavyotumika kwa wagonjwa kopo 12 na barakoa za kawaida pakiti 978 ambavyo vyote vimegaharimu zaidi ya Sh Milioni 29 vilivyonunuliwa katika Bohari ya dawa (MSD),” amesema Shibula.
Akipokea vifaa hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Simon Berege amelipongeza shirika la OXFAM kwa kuiunga mkono serikali katika mapambano dhidi ya COVID 19 na kuahidi kuwa vitatumika ilivyoelekezwa katika kituo maalumu cha uangalizi wahisiwa wa Corona cha Bugarama.

“Niwatoe hofu wananchi katika Halmashauri ya Msalala tangu ugonjwa wa Corona uripotiwe hapa nchini hapajawahi kutokea mtu yeyote anayeumwa ugonjwa huo na hadi hii leo hakuna mgonjwa yeyote katika kituo cha afya Bugarama anayehisiwa kuwa nao,” amesema Berege. 

Nae Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dk. Ernest Chacha amesema kuwa kwa sasa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi hususan katika maeneo yenye mikusanyiko kama vile minada na machimboni ili waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 unaoenezwa na virusi vya Corona.
“Tunaendelea kuwasihi wananchi waendelee kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Waataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka,kupaka vitakasa mikono na barakoa katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ili kuwakinga na virusi hivyo,” amesema Chacha.