Header Ads Widget

WANAFUNZI VYUO, KIDATO CHA SITA WATAKIWA KUJIAMINI NA KUONDOA HOFU


Chuo Kikuu Dodoma : Picha na maktaba
Askofu wa Kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania (IEAGT) la mjini Shinyanga, David Mabushi

Na Kareny Masasy - Shinyanga
Wakati leo Juni mosi, 2020 vyuo na shule za sekondari (kidato cha sita) wakirejea kuendelea na masomo baada ya kusimama kwa takribani miezi miwili kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya Corona, wanafunzi hao wameaswa kuondoa hofu bali wajiamini na kuweka bidii katika masomo yao ili wafanye vizuri kwenye mitihani iliyoko mbele yao.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Askofu Kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania (IEAGT) la mjini Shinyanga, David Mabushi wakati wa mahubiri katika misa ya Jumapili Mei 31, 2020 mbele ya waumini wake, ambapo amewashauri wanafunzi waondoe hofu na wasimamie vizuri masomo yao.

Askofu Mabushi alisema kuwa Serikali imekwisha chukua hatua ya kuwakinga wanafunzi dhidi ya maambukizi ya Corona kwa kuzingatia maekelekezo ya wataalamu wa afya, hivyo ni jukumu la wanafunzi kutimiza matakwa hayo na waache kuiendekeza hofu kuwatawala kwani hofu ni adui mkubwa katika kitu chochote.

“Serikali inawafuatilia kwa ukaribu kuangalia usalama wao hivyo wasiwe na hofu wajitahidi kusoma kwa bidii nakusahau masuala ya likizo ya Corona ili waweze kufaulu vizuri katika mitihani yao wanayotarajia kuifanya mwezi ujao,”alisema Askofu Mabushi.

Askofu Mabushi alisema kuwa katika kupambana na maambukizi ya COVID-19 kwa kufanya maombi mfululizo aliipongeza Serikali kwa njia mbalimbali walizotumia kupunguza tatizo hilo, huku akiwahasa waumini kuendelea kufuata masharti ya kupambana na virusi hivyo kwani haujaisha bali maambukizi ndiyo yaliyopungua kwa mujibu wa wataalam.
TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807