Header Ads Widget

UWANJA WA KISASA FRESHO COMPLEX WAANZA KUTUMIKA, SIMBA NA YANGA ZAKARIBISHWA


Muonekano wa eneo la kuchezea la uwanja wa Fresho Complex.
Mchezaji wa timu ya Mwanza Veterans, Rajesh Kotecha akionyesha ufundi wa kumiliki mpira wakati wa mchezo wa bonanza maalum dhidi ya Shinyanga Veterans uliofanyika kwenye uwanja mpya na wa kisasa wa Fresho Complex uliopo eneo la Bugweto mjini Shnyanga. Timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana mabao 3-3.  

Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club blog
Hatimaye uwanja wa Kisasa wa mpira wa miguu ulioko eneo la Bugweto kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga unaojulikana kwa jina la Fresho Complex, umeanza kutumika rasmi leo Juni 6, 2020 kwa michezo ya bonanza lililozikutanisha timu nne za maveterani kutoka mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa.

Bonanza hilo lililoanza leo asubuhi lilifunguliwa na Kamanda wa Base ya Shinyanga, Kanali Justus Kita, likiwa na lengo la kuzikutanisha timu hizo na kutoa fursa ya wanamichezo kufanya mazoezi kuimarisha afya na kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.

Akizindua bonanza hilo, Kanali Kita alisema uwekezaji huo ni jambo jema na ni fursa nzuri kwa wanamichezo, kwani ni hospitali na tiba kwao, hivyo uwepo wa uwanja huo ni hamasa kwa wana michezo.
Kamanda wa Base ya Shinyanga, Kanali Justus Kita akizungumza baada ya kufungua bonanza hilo.

Akizungumzia ujenzi wa uwanja wa Fresho Complex unaomilikiwa na mwekezaji mzawa, Fredy Shoo kupitia kampuni yake ya Fresho Investment Co. Ltd, Meneja wa uwanja huo, Ombeni Kweka alisema eneo la kuchezea (Pitch) limekamilika kwa asilimia 100 na limeanza kutumika rasmi, ambapo nyasi za uwanja huo zina asili ya nchini Afrika Kusini lakini zilitolewa Mwadui.
Meneja na Mbunifu wa uwanja wa Fresho Complex, Ombeni Kweka.

Kweka ambaye ndiye aliyebuni uwanja huo ameeleza kwamba mbali na eneo la kuchezea, uwanja huo umekamilika kwa asilimia 25 tu na unatarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 kati ya mwaka 2022 na 2023 ukijumuisha bustani ya matunda, barabara ya kiwango cha lami, hoteli ya nyota tano, ukumbi wenye uwezo wa kuchukua watu 1,000, eneo la kuogelea (Swimming pool) kwa ajili ya watoto na watu wazima.

“Uwanja wetu ni bora na wa Kisasa hakuna wa mfano kwa kanda ya ziwa, katika eneo la kuchezea (Pitch) kuna mfumo wa mabomba yanayomwagilia maji kutoka chini na mfano hii tunaiona Ulaya, lakini pia Ujenzi wa majukwaa ukikamilika utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 18,000 waliokaa na wengine kama 2,000 watakaosimama.

“Tumeanza kuujenga mwaka 2017 upana wake kwa eneo la kuchezea ni 68 kwa 110, sehemu zngine ambazo hazijakamilika ni eneo la kukimbilia (run away), bwawa la samaki, gym na vyumba vya kubadilishia nguo,” amesema.

Kwa upande wake mmiliki wa uwanja huo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Fresho Investment ya mjni Shinyanga, Fredy Shoo, amesema kwamba licha ya eneo la kuchezea kuanza kutumika lakini uwanja huo haujazinduliwa rasmi, na kwamba sababu kubwa iliyomsukuma kuujenga ni nia ya dhati ya Serikali kuhamasisha uwekezaji na kutoa fursa kwa wana michezo kupata sehemu ya kufanyia mazoezi.
Mkurugenzi wa Fresho Investiment Co. Ltd na Mmiliki wa uwanja wa Fresho Complex, Fredy Shoo.

Shoo amesema kuwa uwepo wa uwanja huo ni fursa nzuri kwa wanamichezo wote wa mkoa wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla, ambapo ametoa fursa ya kufanya mazoezi bure kila Jumamosi, lakini pia akazikaribsha timu za ligi kuu na daraja la kwanza kufika wafanye mazoezi ili waweze kuuingizia kipato uwanja huo.

Timu zilizoshirki bonanza hilo ni Mwanza Star Veterans ya Mwanza, Shinyanga Veterans, Jeshi Stars veteran ya Shinyanga na Unyanyembe Veterans ya Tabora, ambapo mchezo wa Ufunguzi ulizikutanisha Jeshi Stars na Unyanyembe zilizotoshana nguvu kwa kufungana mabao 3-3, huku Shinyanga Veterans ikiichapa Mwanza Veterans mabao 3-2 na moja wapo ya bao la ushindi likifungwa na Fredy Shoo.

Mmoja wa wachezaji waliohudhuria bonanza hilo ni Kocha Mkongwe, Athuman Bilal ‘Bilo’ aliyewahi kuzifundisha Toto Africans, Alliance FC, Stand United na kwa sasa akiinoa Gwambina FC ya Misungwi kama kocha Msaidizi, ambapo ameeleza kuwa kujengwa kwa uwanja huo ni hamasa kwa vijana wenye vipaji, timu na fursa kwa makocha kupata ajira na sehemu ya kufanyia mazoezi, hivyo akaomba jitihada hizo ziungwe mkono na wawekezaji wa namna hiyo wazidi kujitokeza kwa wingi. 
Muonekano wa eneo la kuchezea la uwanja huo.
Baadhi ya wachezaj wa timu za Jeshi Stars Veteran ya Shinyanga na Unyanyembe Veterans wakichuana kwenye uwanja wa Fresho Complex mjini Shinyanga, Juni 6, 2020.
Wachezaji wa timu za Jeshi Stars Veteran ya Shnyanga na Unyanyembe ya Tabora wakiwania mpira kwenye mchezo uliozikutanisha timu hizo katika bonanza maalum lililofanyika kwenye uwanja mpya na wa kisasa wa Fresho Complex mjini Shinyanga.Timu hizo zilitoshana nguvu ya kufungana mabao 3-3.
Wachezaji wa Unyanyembe Veterans ya Tabora na Jeshi Stars Veteran ya Shinyanga wakonyeshana uwezo wa kumiliki mpira wakati wa mchezo wa bonanza maalum lililofanyika kwenye uwanja wa kisasa wa Fresho Complex mjini Shinyanga leo Juni 6, 2020.
Benchi la ufundi la tmu ya Jeshi Veteran kifuatilia kwa umakini mchezo wa kkosi chao dhidi ya Unyanyembe Veteran ya Tabora uliopigwa kwenye uwanja wa Fresho Complex na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Mashabiki wa soka wakifuatilia michezo mbalmbali kwenye uwanja wa Fresho Complex.
Sehemu ya wananchi waliohudhuria bonanza hilo na kushuhudia mechi mbalimbali zikichezwa katika uwanja huo.
Wachezaji wa timu za Unyanyembe Veterans na Jeshi Veterans wakichuana kwenye dimba jipya na la kisasa la Fresho Complex la mjini Shinyanga.
Vikosi vya timu za Mwanza Stars Veteran na Shinyanga Veteran vikiwa tayari kwa mchezo.
Kikosi cha Maveterani wa Mwanza (Mwanza Stars Veterans) wakiongozwa na Athuman Bilal 'Bilo' (wa katikati msitari wa mbele waliochuchumaa)
Kikosi cha Shinyanga Veterans kikiongozwa na Fredy Shoo (wa pili kulia waliosimama)
Sehemu ya mashabiki wa soka na wananchi waliohudhuria bonanza hilo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Fresho Investment Co. Ltd na Mmiliki wa uwanja wa Fresho Complex uliopo mjini Shinyanga, Fredy Shoo (kulia) akzungumza na waandishi wa habari.

Picha zote na Kadama Malunde na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog