Header Ads Widget

RAS SHINYANGA AIONYA HALMASHAURI UPOTEVU WA MAPATO, RC TELACK AIKARIBISHA TAKUKURU KUCHUNGUZA




Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela

Na Damian Masyenene – Shinyanga

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga (RAS), Albert Msovela amewajia juu watumishi wa idara ya fedha na Manunuzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa uzembe na kushindwa kusimamia vyema majukumu yao na kupelekea upotevu mkubwa wa fedha, huku akiwapa siku 30 wakuu wa idara hizo kujipima endapo wanastahili kuziongoza.

RAS Msovela alieleza kwamba hafurahishwi na utendaji wa idara hizo kutokana na hoja zilzoibuliwa na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) juu ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo licha ya uwepo wa vyanzo vingi vya mapato.
Ambapo mapato hukusanywa lakini hayapelekwi benki na yanatumiwa na wakusanyaji kutokana na udhibiti hafifu kutoka idara hiyo, hivyo akamuomba Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba kulifanyia kazi na wahusika wachukuliwe hatua hasa kwenye sakata la michango ya watumishi kutopelekwa kwenye mifuko ya hifadhi za jamii licha ya kuchangishwa.

“Bado kuna hoja na majibu mepesi, hoja nyingi zilizoibuliwa zinahusiana na mapato kuna fedha haijakusanywa na nyingine imepotea, hii inamaanisha bado ukusanyaji wa mapato siyo mzuri.

“Halmashauri hii inaongoza katika mkoa wetu kwa kuchakachua mashine za ukusanyaji fedha, watumishi wanakusanya mapato wanatafuna, watu mtaani wanakusanya fedha hawapewi ‘Control number’, kwahiyo kama hatutazingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya serikali hatutasonga mbele,” amesema.

Msovela ameongeza kwa kubainisha kuwa hakufurahishwa na mapungufu yaliyopo kwenye halmashauri hiyo na hayuko tayari kuvumilia mambo yasiyofuata kanuni na taratibu, ambapo alimuomba mkuu wa idara ya uhasibu kusimama katika nafasi yake, huku akikionya kitengo cha Manunuzi kwa umma kutotumika vibaya na kujiingiza kwenye siasa.

Akizungumzia idara zinazolalamikiwa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto za kampuni kutolipa mapato na ushuru, madeni mbalimbali ya kodi na kutokusanya ada mbalimbali za leseni na kufanya kufikisha deni la zadi ya Sh Milioni 450, huku pia halmashauri ikidaiwa Sh Milioni 162 kwa kutopeleka fedha zilizokusanywa kwenye mfumo wa POS.
Kufuatia changamoto hizo RC Telack amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa, Albert Msovela kulifkisha kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) suala la fedha zinazokusanywa na watumishi kutopelekwa benki, huku pia akimuagiza Mkuu wa Polisi wilaya ya Shinyanga (OCD), J. Kafumu na kumpa mwezi mmoja kuwasaka mawakala watatu wanaodaiwa fedha zaidi ya Sh milioni 6 za halmashauri walizopewa mkataba wa kuzikusanya mwaka wa fedha 2014/15.

“Hii ni fedha ya serikali waliikusanya lazima wairudishe, tusilindane kwa maovu 2014 siyo mbali hadi tuweze kufuta deni, tukilindana hivi na wengine watafanya hivyo, OCD lichukue hili liko ndani ya uwezo wenu.

“Idara ya fedha na Manunuzi kila hoja wanaguswa, wamesoma na ni wataalam kwahiyo kutofuata utaratibu ni makusudi na zipo sababu na haya yote yanatokea kwa sababu tunafanya kazi kwa mazoea, nataka niwakumbushe mfuate taratibu vinginevyo hatutaki vilio ukoo wako uje utupigie maggot,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ngassa Mboje (Kulia)

Kamapuni ambazo zilikuwa ni mawakala wa ukusanyaji ushuru wa mazao mwaka 2014/15 ni Eusebio Edward (Sh 5,500,00), Nyakimori Investment (Sh 600,000) na Pijoma Co. Ltd (Sh 330,000) zinazodaiwa jumla ya Sh Mlioni 6,430,000 lakini kwa sasa hazijulikani zilizopo baada ya kutafutwa kwa muda mrefu, jambo ambalo lilipendekezwa kwamba deni hilo lifutwe, lakini RC Telack akakataa na kuagiza watafutwe.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amesema kuwa ili kuhakikisha kwamba mapato hayaendelei kupotea amepigwa marufuku mweka hazina kwenda kuchukua fedha kwenye kata na kutowasilishwa kwenye mifumo rasmi, ambapo aliwataka watumishi wote kufuata taratibu kwani ndiyo wanaokwamisha halmashauri hiyo kusonga mbele huku akiwaonya kuwa wataanza kuitwa mmoja baada ya mwingine kushughulikiwa na kuwajibishwa.



Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (kushoto).

TAZAMA PICHA ZAIDI >>