Header Ads Widget

RC TELACK AWAPA SAA 5 WATUMISHI WALIOKAIDI KUHAMIA ISELAMAGAZI

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto) akizungumza na madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakati wa kikao cha baraza la madiwani kujadli hoja mbalimbali za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) leo Alhamisi Juni 4, 2020.

Na Damian Masyenene – Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ameonyesha kukasirishwa na kitendo cha baadhi ya watumishi wa serikali Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kukaidi maelekezo ya kuondoka mjini (Manispaa) na kuhamia eneo la kazi ilipo halmashauri yao (Iselamagazi).

Ambapo kufuatia kitendo hicho, Mkuu huyo wa mkoa amewapa saa tano kuanzia saa 7:00 mchana hadi 12:00 jioni siku ya Alhamisi Juni 4, 2020 wawe wameondoka na kuhamia kwenye vituo vyao vya kazi vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

RC Telack ametoa maagizo hayo leo Juni 4, 2020 wakati wa kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichoketi kupitia hoja mbalimbali za Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), ambapo kupita kikao hicho aligundua kuwa baadhi ya wakuu wa idara na vitengo hawakuwepo kutokana na kukaa mbali na eneo la kazi.

Hivyo, RC Telack alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hoja Mahiba kumletea orodha ya majina ya watumishi hao na idara za kazi wanazotoka kama hawataripoti/kuhamia Iselamagazi itakapofika kesho (Ijumaa) asubuhi, huku pia akimtaka awasilishe orodha ya majina ya watumishi wote ambao hawakuhudhuria kikao hicho wala kujiandikisha kwenye daftari la mahudhurio.

“Wamekaidi maelekezo ya Rais na wanataka kunijaribu, kwahiyo Mkurugenzi naagiza watumishi wote wanaokaa mjini kufika leo jioni wawe wamehamia hapa (Iselamagazi), ambao hawatahamia nataka kesho asubuhi uniletee majina na idara walizopo.

“Pia watumishi wote ambao hawapo na hawajajisajili kwenye Kitabu cha mahudhurio na wako mjini nataka majina yao, namba za simu na idara wanazotoka,” amesema Mkuu wa Mkoa.

Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakifuatilia kwa umakini hoja mbalimbali wakati wa kikao cha kujadili ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) leo Alhamisi Juni 4, 2020.

Katika upande mwingine RC Telack aliwataka watumishi wote katika halmashauri hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano, kuvunja makundi na kumpa ushirikiano Mkurugenzi, Hoja Mahiba na waachane na propaganda za kutaka aondolewe.

Akizungumzia maagizo ya Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga, Hoja Mahiba, ameyapokea maelekezo hayo na yatafanyiwa kazi mara moja, huku akiwataka watumishi wake kurudi kwenye msitari na kuyatilia maanani yale yote yaliyoelekezwa kwenye kikao hicho.

“Nimepokea maelekezo nitayasimamia ili halmashauri yetu iweze kwenda kwenye msitari unaotakiwa, kwa watendaji wangu nawaambia mwenye masikio na asikie na wajipange kurudi kwenye msitari kama walikuwa wamekengeuka,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga (RAS), Albert Msovela alisema tatizo la watumishi kukatalia mjini limekuwa sugu kwa halmashauri hiyo, ambapo baadhi ya watumishi wamekuwa wakidanganya kuwa wameenda likizo lakini wanapita kwenye vyanzo vya mapato wanakusanya fedha na hawazifikishi kwenye halmashauri hiyo.

“Baadhi ya watumishi bado wanakatalia mjini hawataki kuhamia huku, naagiza Mkurugenzi wakuu wa idara wawe na madaftari ya mahudhurio kuwaona wasaidizi wao, wengine wanasema wameenda likizo kumbe wanazurura kukusanya fedha na hazifiki kwenye halmashauri,” amesema.

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ngassa Mboje alimuomba Katbu Tawala wa Mkoa kuwasaidia kutatua tatizo la upungufu wa madereva wa halmashauri, ambapo kwa sasa wapo 10 peke yake wakati mahitaji ni 21.

“Naomba watumishi turudi kwenye utaratibu siyo vyema tukiwa tunasemana kila siku, tumuombe RAS aendelee kufanya vikao vya kila mara na watumishi kukumbushana wajibu na maeneo ambayo hatujafanya vizuri tuyachukue kama changamoto,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto), Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Ngassa Mboje (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga, Abubakar Mukadamu (kulia) wakfuatilia hoja kwenye kikao cha baraza la madwani wa halmashauri hiyo kilichoketi leo Juni 4, 2020.

Post a Comment

0 Comments