Header Ads Widget

MBATIA: NCCR MAGEUZI IKO TAYARI KUUNGANA NA VYAMA VINGINE UCHAGUZI MKUU 2020

      Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Taifa, James Mbatia

Chama cha NCCR Mageuzi kimefungua milango kwa chama chochote cha siasa nchini, ambacho kipo tayari kushirikiana nacho kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu.

Hayo yamebainishwa jana Juni 4, 2020 na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Alisisitiza kwamba katika uchaguzi mkuu mwaka huu chama hicho kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa kwa maslahi ya taifa. “Niseme tu kwa moyo mmoja, sisi tupo tayari kushirikiana na chama chochote kile cha siasa kwa maslahi ya Mama Tanzania, kwani hata salamu yetu inasema kwa pamoja tutashinda,”amesema Mbatia

Mbatia pia amesema katika uchaguzi mkuu 2020, ajenda yao ni katiba mpya kwani ndiyo kauli ya umma wote. “Ajenda yetu katika uchaguzi huu ni Katiba mpya ni haki yetu kauli hii inatokana na umma wote lazima tutaendelea kuipigania kwa mslahi ya Taifa letu,”amesema Mbatia.

Akizungumzia kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC), amesema kuwa inatakiwa kuzingatia taratibu za kisheria na kikanuni zinafuatwa na maamuzi yanatolewa kwa usawa na haki.

“Uchaguzi Oktoba  tunataka kuliingiza Taifa hili katika historia mpya kwa Tume ya Uchaguzi kutenda haki na usawa,”amesema.

Wakati huo huo, Mbatia amesema chama hicho kitatoa ratiba ya uteuzi wa wagombea urais, wabunge, madiwani pamoja na wawakilishi, mwanzoni mwa wiki ijayo.

Mbatia amesema tayari ameshamwagiza Katibu mkuu wa chama hicho kutoa ratiba ya uteuzi wa wagombea ndani ya chama mapema wiki ijayo. “Nitoe wito kwa vijana na wale wote wenye sifa, kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali, katika uchaguzi huu, katika nafasi za urasi Tanzania Bara na Zanzibar, ubunge, wawakilishi pamoja na zile za udiwani,”alifafanua Mbatia.

Chanzo: TimesMajira

Post a Comment

0 Comments