` MEYA WA MANISPAA YA SHINYANGA SALUM KITUMBO NA NAIBU MEYA PENDO SAWA WAJITAMBULISHA KWA RC MHITA

MEYA WA MANISPAA YA SHINYANGA SALUM KITUMBO NA NAIBU MEYA PENDO SAWA WAJITAMBULISHA KWA RC MHITA

Na RC SHINYANGA.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewapokea rasmi Meya mpya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Salum Kitumbo na Naibu wake Mhe. Pendo Sawa, walipofika ofisini kwake leo Desemba 11, 2025 kwa lengo la kujitambulisha na kuonesha nia ya kushirikiana na ofisi yake katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Manispaa na Mkoa kwa ujumla.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea, RC Mhita aliwapongeza kwa ushindi walioupata na kuwaasa kuwa viongozi wa mfano kwa kutanguliza maslahi ya wananchi.
Alisisitiza umuhimu wa kuwa na maono mapana ya maendeleo na kuwahakikishia ushirikiano wa dhati kutoka ofisi yake.

“Ni matumaini yangu kwamba mtatumia nafasi zenu kusimamia maendeleo ya kweli. Mkoa uko tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha wananchi wa Shinyanga wananufaika na uongozi wenu,” amesema RC Mhita.
Kwa upande wake, Meya Salum Kitumbo alieleza kuwa hatua hiyo ya kujitambulisha ni mwanzo wa ushirikiano wenye tija kati ya Manispaa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Alieleza kuwa lengo lao ni kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati, kwa tija na kwa manufaa ya wananchi wote.

“Tumeona ni jambo la busara kufika mapema kwako Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ili tuanze rasmi safari ya ushirikiano wa kweli kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu,” amesema Mhe. Kitumbo.
Naibu Meya, Mhe. Pendo Sawa naye aliongeza kuwa atakuwa bega kwa bega na Meya katika kuhakikisha kila mwananchi anaguswa na huduma za maendeleo, huku akisisitiza kuwa wapo tayari kupokea maelekezo ya kitaifa na kimkoa kwa ajili ya mafanikio ya Manispaa hiyo.

Mkutano huo umefungua ukurasa mpya wa mahusiano ya kiuongozi katika mkoa wa Shinyanga, ambapo viongozi wote wameonesha dhamira ya dhati ya kutumikia wananchi kwa uadilifu, ushirikiano na uwazi lengo ikiwa ni kirejesha tabasamu kwa wananchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464