Header Ads Widget

PICHA: RC TELACK AWATAHADHARISHA MADIWANI KISHAPU KAMPENI ZA MAPEMA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack


Na Suzy Luhende - Kishapu

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack amewataka madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani hapa kuepuka kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa na serikali wa kufanya kampeni, badala yake wawe na subira muda ukifika watafanya.

Rai hiyo ameitoa Juzi (Jumatano) kwenye kikao cha Baraza la madiwani cha kujadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2018/2019 kilichofanyika wilayani humo.

Telack alisema muda wa kufanya kampeni bado haujafika atakayeonekana anafanya kampeni atachukuliwa hatua za kisheria, hivyo aliwaomba watulie waache kuwa na haraka, na waache kutumia fedha zao ovyo katika nyakati hizi za kuelekea kwenye uchaguzi, kwani kama wamefanya kazi nzuri wananchi ndiyo wataamua.

Pia aliipongeza halmashauri hiyo kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo na kazi zingine za halmashauri hiyo kwani zimefanyika kwa kiwango kinachotakiwa bila kupindisha pindisha.

Hata hivyo aliwaomba madiwani hao waende wakawahamasishe wananchi wanaofanya biashara ndogondogo kununua vitambulisho vya ujasiriamali ili kuepuka kulipa kodi iliyo nje ya uwezo, ikiwemo kuwashauri wananchi kuhifadhi mazao ya chakula kwa ajili ya matumizi ya baadae.
"Nawaomba wananchi waache kuuza mazao mashambani, maana wengine wamekuwa wakiuza mazao yao yakiwa bado shambani, na kusababisha njaa ndani ya familia, hivyo nyinyi madiwani endeleeni kuwapa elimu, na kila mtu ahakikishe anachakula cha kutosha mwaka huu na mwaka kesho, na wale ambao hawakupata wanunue kwani bei kwa sasa iko chini," alisema.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela aliipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa utendaji bora wa kazi, huku akikishauri kitengo cha manunuzi kuhakikisha wanafanya manunuzi kwa kushindanisha ubora na bei ya bidhaa na kuyafanya ndani ya mfumo wa manunuzi wa halmashauri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Boniface Butondo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Lagana alimshukuru uongozi wa mkoa wa shinyanga na kuahidi kuendelea kufanya vizuri kiutendaji ili halmashauri yake iendelee kupata hati safi, ambapo aliowaomba watendaji waendelee kusimamia vizuri miradi mbalimbali ya halmashauri.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Sostenes Mbwilo akiwasilisha hoja za majibu ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka ulioishia June 30, 2019 alisema halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 84 kati ya hizo hoja 33 sawa na asilimia 39 zimetekelezwa kikamilifu.

Na hoja 40 sawa na asilimia 48 ziko katika utekelezaji na majibu yake yamewasilishwa ofisi ya mkaguzi Shinyanga, zikisubiri uhakiki, hoja nne sawa na asilimia tano zimepitiwa, hoja saba sawa na asilimia nane zimerudishwa kwa kuwa zinahitaji majibu ya nyongeza zinasubiri uhakika.

TAZAMA PICHA ZAIDI


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack (kulia) akinawa mikono ili kujikinga na ugonjwa wa Corona wakati wa kuingia kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri ya Kishapu, katikati ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Boniface Butondo akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Sostenes Mbwilo.


Mweka hazina wa halmashauri ya Kishapu, Deus Ngelanizya akisoma taarifa ya matumizi ya fedha kwenye kikao cha Baraza la madiwani cha kujadili majibu ya hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali za mwaka 2018/2019 kilichfanyika wilayani humo.

Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (hayupo pichani) wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG).

TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807