Header Ads Widget

FISI AMSHAMBULIA MTOTO WA MIAKA 2, AFARIKI AKIPELEKWA BUGANDO



Fisi

Na Damian Masyenene – Shinyanga

Mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Charles Christian Makilika (2) mkazi wa Mtaa wa Ugweto Kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga mkoani hapa, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mnyama Fisi akiwa anacheza na watoto wenzake nje ya nyumba yao.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba leo Juni 2, 2020, tukio hilo lilitokea Juni mosi, 2020 saa 1:00 jioni, ambapo mtoto huyo alifikwa na umauti njiani wakati akisafirishwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

Kamanda Magiligimba amesema kuwa mtoto huyo alijeruhiwa na Fisi sehemu za usoni kisha kuburuzwa umbali wa mita 50 ambapo fisi huyo alimuachia baada ya kusikia kelele za wananchi waliokuwa wakimfukuza.

Zaidi Kamanda Magiligimba ameeleza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga.

“Natoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba watoto wako mazingira salama muda wote, wasiachwe peke yao, wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari hasa kwa kipindi hiki ambacho fisi wamekuwa wakionekana maeneo mbalimbali ya mkoa wetu wa Shinyanga,” amesema Kamanda Magiligimba.