Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, akionyesha namba itakayotumiwa kutuma ushahidi wa video, picha na sauti ili kudhibiti wagombea wasiofuata taratibu katika chama hicho.
Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeweka utaratibu wa kuboresha namna ya kusimamia maadili kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu kwa kuanzisha kituo cha taarifa za uchaguzi kitakachosaidia kubaini viongozi wanaolaghai watu kwa kutoa rushwa ili wapigiwe kura.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne Juni 2, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ametoa namba ambazo watu wanaweza kutoa taarifa hizo kwa kutuma ujumbe wa maneno au kutuma ushahidi wa video au sauti katika mtandao wa Whatsapp.
Polepole amesema katika uchaguzi huu rushwa haina nafasi na kwamba chama kiko imara kwenye kusimamia maadali ikiwamo kuwatafuta kokote walipo wanaotumia rushwa kutafuta uongozi.
“Wapo watu wanaojipitisha wilayani na majimboni kwa kigezo cha kuchangisha fomu ya mgombea wa urais, kwa mujibu wa taratibu na mila zetu mgombea wa urais anafahamika, hao wanaochangisha kwa ajili ya fomu ya rais wakamatwe tena muwatolee taarifa kwa vyombo vya dola," amesema.
Aidha ameongeza kuwa ni vema kuwaacha wale ambao bado wanatumikia wananchi wamalize muda wao kwa amani na salama ili kuondoa migongano isiyokuwa na tija ambayo inadhoofisha umoja wa chama hicho.
soma zaidi