Header Ads Widget

WATU 59 WAMENUSURIKA KIFO AJALI YA BASI SHINYANGA






Watu 59 waliokuwa wakisafiri kutoka Jijini Mwanza kwenda Mbeya wamenusurika na kifo mara baada ya basi walilokuwa wakisafiria Premier lenye namba za usajili T, 629 AET, kupata ajali katika kijiji cha Ngaganulwa Usanda wilayani Shinyanga na kusababisha majeruhi Saba.


 Mashuhuda wa wa ajali hiyo Robart Samweli amesema tukio hilo limetokea leo majira ya saa 3 asubuhi katika eneo hilo, ambapo kulikuwa na mabasi mawili yamesimama ndipo basi hilo likiwa katika mwendokasi lilishindwa kusimama na hatimaye dereva kulikwepesha na kuanguka.

Amesema katika eneo hilo kulikuwa na basi la Abood limesimama upande wa kushoto na jingine la Allys upande wa kulia, lilipofika basi hilo la Premier lilianza kufunga break na baada ya dereva kuona limemshinda ndipo akalikwepesha vichakani na kuanguka chini na kuanza kutoa msaada wa kuokoa abiria.

" Pembeni ya barabara kulikuwa na basi la Abood limesimama na upande mwingine kulikuwa na basi la Allys, na basi hili lilikuwa na mwendo kasi lilishindwa kusimama na kusababisha ajali kwani mimi nimeshuhudia kwa macho yangu,” alisema Samweli.

Justice Alyoce mwanafunzi wa kidato cha Sita  ambaye ni mmoja wa abiria alisema wakati wakitoka jijini Mwanza basi hilo la Premier pamoja na Abood yalikuwa yakifukuzana ndipo walipofika eneo hilo na kukuta mabasi la Abooda na Allys yamesimama likamshinda ndipo ikatokea ajali.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Debora Magiligimba ambaye alikuwa eneo la tukio, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi, ambapo dereva wa basi la Premier alipofika eneo hilo na kukuta mabasi mawili yamesimama pande zote basi lilimshinda na hatimaye kuanguka.

Aliwataja majeruhi saba wa ajali hiyo kuwa ni Thabiti Abdul, Swaum Kisandu, Mohamed Nyerere, Betha Minami, Mohamed Ahmed, Ilham Yahya, pamoja na Haida Hassani.

Alisema Majeruhi hao wote wamepata majeraha katika maeneo mbalimbali ya viungo vyao vya miili yao, ambapo walikimbizwa kupatiwa matibabu katika kituo cha afya Tinde kilichopo karibu na eneo la ajali, huku kukiwa hakuna kifo hata kimoja, na kubainisha wanamtafuta dereva wa basi hilo ambaye amekimbia kusikojulikana.


TAZAMA PICHA HAPA CHINI



Basi la Premier lenye namba za usajili T, 629 AET linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Mbeya likiwa limepata ajali katika eneo la Ngaganulwa- Usanda wilayani Shinyanga na kusababisha majeruhi Saba.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga Debora Magiligimba akiwa eneo la tukio akizungumzia chanzo cha ajali hiyo.

Abiria Justice Aloyce ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha Sita Jijijni Mbeya akielezea namna ajali ilivyoanza kutokea kutokana na uzembe wa dereva tangu walivyotoka  Jijini Mwanza.

Muonekano wa basi la Premier likiwa limeanguka chini mara baada ya kupata ajali.

Na Marco Maduhu- Shinyanga.