Header Ads Widget

VPL, FA KUPIGWA DAR, FDL,SDL KUHITIMISHWA MWANZA.




MWONEKANO WA JUU WA UWANJA WA TAIFA JIJINI DAR.
  
Na DAMIAN MASYENENE

SIKU moja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kuruhusu Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), Daraja la Kwanza (FDL) na la Pili (SDL) kurejea ifikapo Juni Mosi, Mwaka huu kumalizia michezo iliyosalia baada ya kusimama kwa takribani miezi miwili, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanika utaratibu na viwanja vitakavyotumika.

Akiweka wazi utaratibu wa namna ya kumalizia michezo hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema kuwa kwa michezo ya Ligi Kuu (VPL) na Kombe la Shirikisho (FA) itachezwa jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Taifa, Uhuru na Azam Complex (Chamazi).

Dk. Mwakyembe amesema kwa michezo ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na la Pili (SDL) itachezwa jijini Mwanza katika viwanja vya CCM Kirumba na Nyamagana.

Katika hatua nyingine Wizara hiyo imebainisha kuwa mechi zote zitachezwa bila mashabiki ila kikundi cha mashabiki 20 kitaruhusiwa kuingiwa uwanjani.

Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) msimu huu ilisimama kupisha wachezaji kujikinga na Virusi vya Corona, huku Wekundu wa Msimbazi Simba SC wakiwa wakiwa na alama 71 kileleni baada ya kucheza michezo 28, Azam FC katika nafasi ya Pili na alama zao 54, Yanga SC katika nafasi ya tatu na alama 51 baada ya michezo 27 na Namungo FC alama 50 katika nafasi ya nne.

Huku Alliance FC wakiwa katika nafasi ya 18 na alama zao 29, wakifuatiwa na Mbao FC katika nafasi ya 19 na pointi 22 na Walima Alzeti Singida United wakishika mkia na alama zao 15 baada ya kushuka dimbani mara 29, ambapo msimu huu zinatarajiwa kushuka daraja timu nne.