Header Ads Widget

KIONGOZI WA UPINZANI NCHINI BURUNDI KUPINGA MATOKEO YA UCHAGUZI WA URAIS




Kiongozi wa Upinzani nchini Burundi Agathon Rwasa ambaye alikuwa wa pili katika uchaguzi wa urais nchini humo ameapa kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Akizungumza na BBC, Bwana Rwasa amesema hakubaliani kabisa na matokeo aliyoyapata, akidai uchaguzi ulitawaliwa na wizi wa kura.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini Burundi,Bwana Evariste Ndayishimiye kutoka Chama tawala cha (CNDD-FDD) na mshirika wa rais wa zamani Pierre Nkurunziza ndiye aliyepata ushindi kwa 68,72% ya kura zilizopigwa huku Bwana Agathon Rwasa kutoka chama cha upinzani cha (CNL)akipata 24,19% ya kura.

Kulingana na sheria za Burundi mgombea asiyekubaliana na matokeo huwasilisha pingamizi la matokeo katika muda usiozidi saa 48 baada ya matokeo kutangazwa.

Bwana Rwasa amesema: "Tunakataa matokeo ya uchaguzi, na tutawasilisha shitaka letu mahakamani…Kama mahakama ya Burundi isipotusikiliza tutawasilisha mashitaka yetu katika Mahakama ya Afrika Mashariki.

"Katika uchaguzi huu tulionewa, tulipigwa baadhi wamefungwa na wengine waliuawa, hayo yote ni ushahidi kwamba matokeo haya yaliyopatikana ndiyo waliyokua wanayataka ".

Rwasa anasema kuwa kipindi cha miaka 15 ya utawala CNDD-FDD kilitawaliwa na unyanyasaji dhidi ya wale wenye mitazamo tofauti na utawala kisiasa.

Aliongeza kuwa : "Ni utawala uliovuruga uchumi, ulivuruga vitu vyote pamoja na uhusiano na nchi nyingine, Warundi ni kama tuko peke yetu…Warundi wamechoshwa na hayo

"Katika uchaguzi huu Warundi walionyesha utashi wao, ndio maana tunaomba chaguo lao liheshimiwe ".

BBC ilijaribu kuzungumza na upande wa chama tawala cha CNDD-FDD kuhusu matokeo ya kura lakini hadi sasa haijawezekana.

Hata hivyo kupitia ukurasa wake wa Twitter Chama cha CNDD-FDD kiliandika "Watu wote wanaomuunga mkono Nayishimiye wanaelekea kuandika ukurasa mpya wa maisha ya Warundi na Burundi".

Orodha ya wagombea wa urais Burundi kulingana na matokeo ya kura:
Evariste Ndayishimiye (CNDD-FDD) - 68.72%
Agathon Rwasa (CNL) - 24.19%
Gaston Sindimwo (UPRONA) - 1.64%
Domitien Ndayizeye (Kira Burundi) - 0.57%
Léonce Ngendakumana (FRODEBU) - 0.47%
Nahimana Dieudonné - 0.42%
Francis Rohero - 0.20%

Bwana Rwasa anasema kuwa Evariste Ndayishimiye ni mtu aliye tayari kushirikiana na wapinzani.

Lakini anasema: "Lakini akiona kwamba Warundi wote wako sawa tutashirikiana lakini akiendelea na njia yao mambo hayatakua rahisi ".