Header Ads Widget

NUMET KUNUSURU AJIRA 178 MGODI WA NORTH MARA


 Na Damian Masyenene.

Chama cha Wafanyakazi wa tasnia ya Madini na Nishati Tanzania (NUMET) kimeeleza kwamba kimeanza kufanya mazungumzo na Mgodi wa North Mara Gold Mine ili kunusuru hatma ya ajira za wafanyakazi 178 waliotangazwa kupoteza nafasi zao hivi karibuni.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 24 na Katibu Mkuu wa NUMET Tanzania, Nicomedes Kajungu na kuchapishwa kwenye ukurasa wa mtandao wa Facebook wa chama hicho, imeeleza kwamba tangazo la kuachishwa kazi kwa wafanyakazi hao ni hatua ngumu kwao hasa kipindi hiki ambacho dunia inapambana na ugonjwa hatari wa Corona.

"Hii ni hatua ngumu kwa wafanyakazi hasa  katika kipindi hiki cha janga la Covid19 ambapo dunia nzima hakuna ajira mpya zinazotengenezwa kwahiyo watu hawa wanapaswa kwenda kukaa tu majumbani kwao," amesema Kajungu.

"Tunaendelea kufanya majadiliano na mwajiri kwa lengo la kunusuru ajira za wafanyakazi hawa," anasema Kajungu.

Taarifa hiyo yenye kichwa cha habari 'TAARIFA YA UPUNGUZAJI WAFANYAKAZI KATIKA MGODI WA NORTH MARA KWA WANACHAMA NA WADAU' imesema kwamba Februari na Machi 2020 kampuni ya North Mara Gold Mine inayomilikiwa kwa ubia na Kampuni ya Barrick Gold Corporation na Serikali ya Tanzania, ilipunguza wafanyakazi 110 kwa sababu kwamba baada ya ubia mpya na serikali wanajipanga upya ili waendeshe kwa faida na kwasababu hiyo, kuna majukumu yanarudi serikalini na kusababisha baadhi ya wafanyakazi kukosa ajira.

Taarifa iliendelea kunukuu kwamba  Mei 2, mwaka huu Kampuni hiyo kwa mara nyingine ilitangza upunguzaji wa wafanyakazi 178 ikielezwa kuwa sababu ni bwawa la maji yanayotunza maji yanayotoka kwenye mtambo wa kuchakata dhahabu (Tailings  Storage Facillities) limejaa na kufurika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Kwasababu hiyo, wamelazimika kuyahamishia maji hayo kwenye moja ya shimo (Pit) walilokuwa wanaendeleza uchimbaji wa dhahabu. Kwasababu hiyo, wafanyakazi wote wanaofanya kazi katika shimo  hilo wanapoteza ajira zao.

Kajungu amesema kwamba wataendelea kuwajulisha wanachama wake juu ya kinachoendelea katika mazungumzo hayo kadri wanavyosonga mbele katika majadiliano.

Chanzo -Ukurasa wa Facebook wa NUMET-Tanzania
.