Header Ads Widget

JPM KUKATAA LOCKDOWN NA TAARIFA ZA HOFU KUMESAIDIA KUPIGA VITA CORONANa Mwandishi wetu

Imeelezwa kwamba msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kuamua kupita njia ya kipekee na kuwa na maamuzi tofauti na mataifa mengine yote duniani katika kutafuta ufumbuzi wa Mapambano ya  virusi vya Corona ikiwemo kukataa kupitisha uamuzi wa kuwafungia watu ndani ‘Lockdown’ umelisaidia taifa kupiga hatua kubwa katika mapambano hayo ya ugonjwa wa COVID-19.


Hayo yameelezwa na Askofu wa Kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania (IEAGT) la mjini Shinyanga, Askofu David Mabushi leo Mei 24, 2020 katika ibada ya Jumapili Kanisani hapo ambapo ameipongeza Serikali kwa njia walizotumia kupunguza maambukizi ya COVID-19  kwa kuwa tofauti sana na dunia nzima kupitia ushauri wa shirika la afya dunia WHO
.
Mabushi amesema kuwa kutowafungia watanzania majumbani (lockdown) na kuwaondolea wananchi hofu kwa kubana taarifa za hali ya maambukizi imesaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.

“Tuliona mitazamo ya wanasayansi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na wanasiasa wengi wa dunia wakilazimisha watu wafungiwe ndani lakini njia hizo zimesababisha dunia nzima kupata shida tofauti na taifa letu lililochagua mbinu nyingine.

“Nampongeza sana Rais wetu kwa njia alizotumia kupambana na janga hili, tunaona kwa sasa hata mataifa mengi ya dunia yameanza kufungua mipaka yao na wengine kuruhusu shughuli za ibada kuendelea kama kawaida,” amesema Askofu Mabushi.

Askofu Mabushi ameongeza kwa kusema kuwa kukaa Majumbani bila shughuli yoyote kuna changia kupunguza kinga za mwili, huku utoaji wa taarifa nyingi zenye kujenga hofu kwa wananchi kuna sababisha wananchi kufariki kwa hofu.

Kwa upande wao baadhi ya waumini wa Kanisa hilo akiwemo   Leonard Kajiba na Neema Elias wameupongeza uamuzi wa Rais wa Kutoifungia nchi kwani kungesababisha jamii kubwa ya watanzanai kuteseka kutokana na wengi wao hutegemea kutoka nje kufanya shughuli mbalimbali na kujipatia kipato kwa ajili ya maisha yao ya  kila siku.

Ibada hiyo ni sehemu  ya  siku tatu zilizotengwa kwa ajili ya  kumshukuru Mungu kwa kuliepusha  taifa na Maambukizi  makubwa ya Corona kutokana na idadi ndogo ya maambukzi ya Covid- 19.

Ibada hiyo ambayo imetumika kwa waumini wa kanisa hilo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulisaidia taifa la Tanzania kuvuka salama katika kipindi hiki kigumu baada ya kusali na kuomba kwa miezi kadhaa, ambapo pia Serikali ilitenga siku tatu kwa wananchi kumshukuru Mungu.
TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807