📌 Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa sera hizo;
📌 Waziri Kapinga afanya mkutano na waandishi wa habari kueleza hatua ya maandalizi iliyofikiwa;
📌Asema Serikali inalenga kuongeza mchango wa sekta ya viwanda hadi kufikia asilimia 15 kwenye pato la Taifa;
📌 Asema Sera ya maendeleo endelevu ya viwanda na Sera ya maendeleo ya jasirimali dogo na kati kuinua biashara bunifu la makundi yote.
DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara inatarajia kuzindua sera mbili mpya zinazolenga kuimarisha maendeleo ya sekta ya viwanda na jasiriamali ndogo na za kati nchini ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuongeza uzalishaji, ajira, uongezaji thamani wa malighafi za ndani na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 31, 2026, katika Ukumbi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), jijini Dar es Salaam, Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema Sera hizo ni Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya jasiriamali ndogo na za Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la Mwaka 2025).
Amesema Sera hizo zimefanyiwa mapitio ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kuweka mazingira wezeshi ya biashara, uwekezaji na uzalishaji nchini na kuongeza kuwa zitaimarisha pia mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.
Mhe Kapinga aliongeza kuwa Serikali inalenga kuongeza mchango wa sekta hiyo hadi kufikia asilimia 15 ya Pato la Taifa, sambamba na kuongeza uzalishaji, uongezaji thamani wa malighafi za ndani na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Waziri Kapinga amesema Wizara imejipanga vizuri kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kuhakikisha kila sekta inajipanga na kujiratibu upya ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Aidha, Waziri Kapinga amesema Serikali inaendelea kuimarisha na kuitangaza nembo ya Made in Tanzania kwa lengo la kuongeza utambuzi na kuaminika kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, kukuza matumizi ya bidhaa za ndani na kupanua fursa za masoko kwa wazalishaji wa Kitanzania.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhamasisha wananchi kuthamini bidhaa za ndani na kuimarisha ushindani wake katika masoko ya kimataifa.
Kwa upande wa maendeleo ya wajasiriamali wadogo na wa kati, Waziri Kapinga amesema Sera husika inalenga kuboresha miundombinu wezeshi, kuongeza upatikanaji wa mitaji, kukuza matumizi ya teknolojia na ubunifu pamoja na kurahisisha upatikanaji wa masoko kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa na wajasiriamali hao ma hatua hiyo inalenga kuwawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao, kuongeza tija na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kwa upande wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda, amesema inalenga kuongeza thamani ya mazao na rasilimali zinazozalishwa nchini kupitia uimarishaji wa mnyororo wa thamani, kuendeleza viwanda vya kimkakati, kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na kuimarisha uwezo wa viwanda vya ndani kushindana katika masoko.
Aidha, sera hiyo inalenga kuchochea uwekezaji katika sekta ya viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Kuelekea uzinduzi huo, Wizara ya Viwanda na Biashara imeandaa maonesho na kliniki za biashara Novemba 2 na kongamano la wadau wa sekta ya Viwanda na Biashara wanatarajia kukutana Novemba 3, 2026, kwa lengo la kuwapa wadau wa sekta ya viwanda na biashara fursa ya kujifunza kuhusu sera hizo, kujadili masuala ya utekelezaji na kuelewa mchango wao katika kuimarisha maendeleo ya viwanda na ujasiriamali nchini.
Uzinduzi rasmi wa Sera hizo utafanyika Novemba 4, 2026, jijini Dodoma, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.







