` CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA KIMEFANYA KIKAO CHA 45 CHA BUNGE MKOANI SHINYANGA, KESHO KUFANYA UCHAGUZI WA VIONGOZI WAPYA

WANDAMAN HOTEL

CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA KIMEFANYA KIKAO CHA 45 CHA BUNGE MKOANI SHINYANGA, KESHO KUFANYA UCHAGUZI WA VIONGOZI WAPYA



CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA KIMEFANYA KIKAO CHA 45 CHA BUNGE MKOANI SHINYANGA, KESHO KUFANYA UCHAGUZI WA VIONGOZI WAPYA

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania kimefanya kikao cha 45 cha Bunge la wanafunzi mkoani Shinyanga, kilichowakutanisha wawakilishi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Kikao hicho cha siku tatu kilichoanza jana kinatarajiwa kuhitimishwa kesho, Oktoba 16, kwa kufanya uchaguzi wa viongozi wapya wa Serikali ya Wanafunzi, wakiwamo Rais, Makamu wa Rais na Katibu Mkuu.

Akizungumza leo Oktoba 15, 2026, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Felix Rugeyamu, ambaye anamaliza muda wake wa uongozi kesho baada ya uchaguzi na kupatikana kwa viongozi wapya, amesema kikao hicho kimejadili masuala mbalimbali ya kitaifa, huku uchaguzi wa viongozi wapya ukiwa miongoni mwa shughuli muhimu zinazotarajiwa kufanyika kesho.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wao, waliweza kuwalipia ada wanafunzi zaidi ya 150 waliokuwa na changamoto ya kulipa ada, na hivyo kuwawezesha kukamilisha masomo yao.

“Tamaduni zetu za Kitanzania na katika vyuo vyetu, ni nadra kusikia Serikali ya Wanafunzi imewalipia wanafunzi wenzao ada ili waweze kuhitimisha masomo yao. Tumefanya hivyo kwa sababu Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni tofauti na vyuo vingine vyote,” amesema Felix.
Aidha, amewataka viongozi watakaochaguliwa kuongoza serikali hiyo kuhakikisha hawaongozwi na mihemko, kupenda mijadala na maandamano au mitazamo ya kizazi cha sasa kinachojulikana kama Gen Z, bali wawe viongozi wenye hekima na ukomavu, wanaosimamia maslahi mapana ya wanafunzi bila kukiuka heshima ya menejimenti ya chuo.

Naye mgeni rasmi, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Josiah Katani, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Alex Makulilo, amesema viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wanapaswa kuwa kiungo muhimu katika kujenga mahusiano mazuri kati ya wanafunzi na menejimenti ya chuo.
Amesema hali hiyo inaweza kufikiwa kwa kutumia majadiliano yenye kujenga, kuheshimiana na kufuata taratibu zilizowekwa.

Aidha, amewataka viongozi wapya watakaochaguliwa kutambua kuwa wanapoingia katika baraza, wanakuwa wajumbe sawa na wengine. Hivyo, wanapaswa kushiriki katika kufanya maamuzi yanayozingatia maslahi ya wanafunzi, chuo na taifa kwa ujumla, badala ya kulifanya baraza kuwa chombo cha kushindana na uongozi wa chuo.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania walioshiriki katika mkutano huo, akiwamo Caroline Robson, wameupongeza uongozi wa Serikali ya Wanafunzi unaomaliza muda wake kwa kujali mahitaji ya wenzao walioshindwa kulipa ada.

Wametoa wito kwa uongozi ujao kufuata nyayo hizo kwa kuendelea kujali mahitaji ya wanafunzi na kushughulikia changamoto zinazowakabili.

TAZAMA PICHA👇👇
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Profesa Josiah Katani, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Alex Makulilo, akizungumza kwenye kikao hicho.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Profesa Josiah Katani, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Alex Makulilo, akizungumza kwenye kikao hicho.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Felix Rugeyamu, akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464