Na Marco Maduhu, DODOMA
Waandishi wa habari wametakiwa kupaza sauti za wananchi wa vijijini, na kwamba asilimia 65 ya watanzania wanaishi katika maeneo hayo, ili kuibua matatizo yao, kusaidia kupata ufumbuzi na kuchochea maendeleo.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 31, 2026, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Gerson Msigwa, wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini (RUJAT).
Amesema, zaidi ya asilimia 80 ya vyombo vya habari vipo mijini na mara nyingi huandika habari zinazohusu maeneo hayo, licha ya ukweli kwamba zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanaishi vijijini. Hivyo, amewataka waandishi wa habari kujikita zaidi katika kuandika habari za vijijini kwa kuwa ndiko kunakoishi sehemu kubwa ya Watanzania.
“Mwandishi wa habari ni sauti ya wananchi, mnapaswa kusifiwa na wananchi kwa kuandika habari zenye kuleta matokeo chanya kwao kwa kutatua shida zao,” amesema Msigwa.
Pia, amewataka waandishi hao kufanya utafiti kabla ya kuandika habari, pamoja na kuandika habari za uchunguzi, bila kusahau kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Katika hatua nyingine, amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika habari zinazolinda amani ya nchi.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari, akibainisha kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anawapenda waandishi wa habari na kuunga mkono uhuru wa habari.
Naye Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya, ambaye pia ni mwandishi wa habari mwandamizi, amepongeza kuanzishwa kwa chama hicho cha waandishi wa habari za vijijini, akisema kitasaidia kupaza sauti za wananchi wa maeneo hayo.
Kwa upande wake, Katibu wa chama hicho, Prosper Kwigize, akiwasilisha taarifa ya chama kwa Msigwa, amesema chama hicho kilianzishwa mwaka 2020 na hadi sasa kina wanachama zaidi ya 120.
Amesema malengo ya chama hicho ni kuandika habari za vijijini kwa kuwapa sauti wananchi wa maeneo hayo, pamoja na kuzalisha maudhui bora yanayochochea mijadala na kuleta matokeo chanya.
TAZAMA PICHA👇👇
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Gerson Msigwa akizungumza.
Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya akizungumza.
Mwenyekiti wa RUJAT Neville Meena akizungumza.
Katibu wa RUJAT Prosper Kwigize akiwasilisha taarifa ya RUJAT.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464






















