` RISASI NA KAHAMA SIXERS KUPAMBANA FAINALI YA MWISHO KUWANIA UBINGWA

WANDAMAN HOTEL

RISASI NA KAHAMA SIXERS KUPAMBANA FAINALI YA MWISHO KUWANIA UBINGWA


Na Stella Herman, Shinyanga

Timu ya mpira wa kikapu ya Risasi ya Wilaya ya Shinyanga imeibuka na ushindi wa pointi 77-55 dhidi ya Kahama Sixers katika mchezo wa pili wa fainali ya Mashindano ya Mpira wa Kikapu ngazi ya Mkoa wa Shinyanga uliochezwa mjini Shinyanga.

Ushindi huo umeifanya Risasi kusawazisha matokeo ya fainali hizo baada ya Kahama Sixers kushinda mchezo wa kwanza uliochezwa wilayani Kahama.

Kabla ya mchezo huo, Kahama Sixers ilikuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa wa msimu huu mapema endapo ingeibuka na ushindi katika mchezo wa pili lakini Risasi imefanikiwa kuzuia hilo baada ya kupata ushindi wa pointi 77 dhidi ya 55.

Mchezo huo umevuta hisia za mashabiki wa mpira wa kikapu waliojitokeza kwa wingi kushuhudia ushindani wa timu hizo mbili, huku kila upande ukipambana kutafuta ushindi muhimu kuelekea ubingwa wa msimu huu.

Akizungumza baada ya mchezo huo Kocha wa Kahama Sixers Endrwe Mpemba amebainisha namna walivyojipanga na timu yake kuelekea fainali ya mwisho, ambapo amesema katika mchezo huo wameshindwa kuchukuwa kombe lakini wanaamini mchezo ujao wa fainali ya tatu ambayo itakuwa ya mwisho wataibuka washindi.

Aidha,ameipongeza timu ya Risasi ya Shinyanga kwa kupata ushindi katika fainali ya pili na amebainisha mchezo huo ulikuwa mzuri licha ya wao kupoteza.

Kwa upande wake Kocha wa timu ya Risasi Godfrey Timalya, amesema ushindi huo umeipa timu yake nafasi ya kuendelea kupambana katika mbio za kuwania ubingwa wa Mkoa wa Shinyanga kwa mwaka 2026 na wanatumaini watachukuwa ubingwa

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Shinyanga Yohana William, amezungumzia ushindani uliopo katika mashindano hayo pamoja na mwitikio wa mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo na kubainisha kuwa mpambano ulikuwa mkali kutokana na timu zote zilikuwa zimejipanga.

Amesema fainali ya tatu itachezwa Kahama Oktoba 11, 2026 na timu itakayoshinda itapewa kombe na kutangazwa rasmi kubwa bingwa wa msimu huu.
Mgeni rasmi katika mchezo huo Abdulazizi Sakala amesema mashindano hayo yanatoa fursa kwa mashabiki kubata burudani na kuona mafanikio ya timu zao,huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya mchezo wa mpira wa kikapu mkoani Shinyanga.









Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464