
KONGAMANO LA MISA TAN NA WADAU 2026 KUONGEZA KASI YA UKUAJI WA
UCHUMI WA NCHI KISEKTA
Na Marco
Maduhu, MWANZA
Kongamano la Taasisi ya Vyombo vya
Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), na wadau mwaka 2026,
limetajwa kuwa kichocheo muhimu cha kukuza uchumi wa nchi na kuongeza pato la
mwananchi mmoja mmoja.
TAZAMA VIDEO👇👇
Kongamano hilo limefanyika leo, Oktoba
12, 2026, jijini Mwanza, likihusisha baadhi ya waandishi wa habari na wahariri
kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Kigoma na Mara, pamoja na wadau
kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa
Umma (PSSSF), Shirika la Meli Tanzania (TASHICO), Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), TANAPA, Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), TBL, SBC
na Idara ya Uhamiaji.
Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya
Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda,
akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CP Salum Hamduni, ambaye
alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo, amesema ni la
muhimu kuhabarisha umma ili utambue fursa mbalimbali za kiuchumi.
Machunda amesema utekelezaji wa mipango
ya maendeleo ya uchumi wa nchi unahitaji ushirikiano wa karibu miongoni mwa
wadau mbalimbali, wakiwamo Serikali, sekta binafsi na waandishi wa habari.
“Wananchi wana haki ya kufahamu kupitia
vyombo vya habari miradi ya maendeleo inayotekelezwa na taasisi mbalimbali za
Serikali. Utayari wa taasisi hizo kushirikiana na MISA TAN ni dhamira ya dhati
ya kupanua wigo wa ushirikiano na kuwajengea uwezo wanahabari ili waweze
kuripoti kwa weledi utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi inayotekelezwa
nchini. Hatua hiyo itachangia kuinua pato la taifa na la mwananchi mmoja
mmoja,” amesema Machunda.
Aidha, amewataka waandishi wa habari
kuandika taarifa zao kwa weledi, kuzihariri kwa kina na kuepuka kuandika
taarifa zinazoweza kusababisha taharuki, huku wakizingatia maadili ya taaluma
yao.
Naye Mwenyekiti wa MISA TAN Edwin Soko,
amesema kongamano hilo ni muhimu katika kusukuma maendeleo kupitia sekta ya
habari, kwa sababu waandishi wa habari wana nguvu ya kuzalisha maudhui na
kuweka ajenda zinazosaidia kufahamu vipaumbele vya nchi na kuwaelimisha
wananchi kuhusu namna Serikali inavyotekeleza majukumu yake.
“Vyombo vya habari vina nguvu ya kutengeneza mwelekeo wa taifa,” amesema Soko.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya
Sita, chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa mdau mkubwa katika
kuhakikisha kunakuwa na mazingira salama na wezeshi kwa vyombo vya habari.
Amesema hivi karibuni Serikali ilifanya
mapitio ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 (Media
Services Act, 2016), pamoja na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2018.
Amesema miongoni mwa marekebisho yaliyofanyika ni kupunguzwa kwa ada ya usajili
wa blogu kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000, jambo alilolitaja kuwa mafanikio
makubwa yanayotokana na ushirikiano kati ya Serikali ya Awamu ya Sita na vyombo
vya habari.
Ameongeza kuwa Rais Samia alipoingia
madarakani, alifungulia magazeti yaliyokuwa yamefungiwa, hatua ambayo amesema
imekuwa faraja kubwa kwa wadau wa habari. Pia, amepongeza kuendelea kutambuliwa
kwa kazi za waandishi wa habari kupitia tuzo za Samia Kalamu Award.
Katika hatua nyingine, Soko amewataka waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma, pamoja na kuandika habari zinazozingatia maslahi ya taifa.
PICHA NA KADAMA MALUNDE NA SUMAI SALUM👇👇


















































































































