` BARRICK NORTH MARA YAFANIKISHA UJENZI WA SHULE MPYA YA MSINGI KERENDE

WANDAMAN HOTEL

BARRICK NORTH MARA YAFANIKISHA UJENZI WA SHULE MPYA YA MSINGI KERENDE

 



Muonekano wa mbele wa majengo ya Shule mpya ya Msingi Mgosi katika Kijiji cha Kerende, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, iliyojengwa kwa ufadhili wa Mgodi wa Barrick North Mara kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Muonekano wa moja ya vyoo vilivyojengwa katika Shule mpya ya Msingi Mgosi, Kijiji cha Kerende, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, kupitia ufadhili wa Mgodi wa Barrick North Mara kwa mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kerende, Mussa Magaigwa, akieleza manufaa ya ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Mgosi, inayotarajiwa kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

**

#Itaondoa adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta elimu

Wilayani Tarime katika mkoa wa Mara utekelezaji wa miradi ya elimu kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaendelea kwa kasi na kufungua milango ya fursa, usalama na kuleta matumaini mapya.

Katika kufanikisha  dhamira yake ya uwajibikaji katika uchimbaji madini na kuendeleza jamii zinazozunguka maeneo ya mgodi, Barrick North Mara imejenga shule mpya ya msingi katika kijiji cha Kerende kilichopo kata ya Kemambo ambayo itawapunguzia wanafunzi adha ya kutembea mwendo mrefu kutafuta elimu na kuwawezesha kusoma katika mazingira bora na salama.

Kijiji cha Kerende kina vitongoji 10 ambapo wanafunzi kutoka vitongoji vitatu vya Mgosi, Isakahembe na Nyanyoka watakuwa wanufaika wa shule hiyo mpya  ambayo itakuwa ya nne katika kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 8,000 na imepewa jina la Mlima Mgosi ambao ni moja ya kivutio  kilichopo  kijijini hapo.

Mradi wa ujenzi wa shule hiyo ulianza Juni 2025 na mkandarasi wake aliukabidhi kwa Serikali ya Kijiji hicho Januari 2026 na taarifa zilizopo zinasema maandalizi ya kufungua shule hiyo yapo katika hatua za mwisho na wakati wowote itafungua milango kwa mamia ya wanafunzi ambao watahamishwa kutoka shule nyingine zilizopo katika kijiji hicho.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kerende, Marwa Gabogwe, ameeleza kuwa mradi huu wa kuboresha elimu kijijini hapo umeenda vizuri na utafanikisha kuwezesha wanafunzi wengi kujiunga na elimu ya shule ya msingi na kwa kiasi kikubwa umewaondolea adha wanafunzi wa kijiji hicho kutembea umbali wa mwendo mrefu kutafuta elimu katika shule zilizopo vijiji vya mbali.

Shule nyingine za msingi za serikali zilizopo katika kijiji hicho ni Kerende, Ngeng’e na Ntimaro.

 Shilingi zaidi ya milioni 300 zimetumika katika kutekeleza mradi huo ambao umehusisha ununuzi wa uwanja wa eneo la shule (ekari 10), ujenzi wa vyumba sita vya madarasa, ofisi ya walimu, vyoo vya walimu, wanafunzi na uwanja wa mpira.

Utekelezaji wa mradi huo pia umejumuisha utengenezaji wa madawati ya wanafunzi 125 ambayo yapo tayari yakisubiri wanafunzi watakaofungua pazia katika shule hiyo.

Wakazi wa kijiji cha Kerende wanatoa shukrani kwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals kwa kutoa fedha ambazo zimefanikisha ujenzi wa shule hiyo kupitia utekelezaji wake wa sera ya CSR kwa vitendo. 

“Mradi huu ulikuwa hitaji kubwa kwa sababu kijiji chetu kina vitongoji 10 na wanafunzi ni wengi. Hivyo, itakuwa na msaada mkubwa kwa watoto wetu,” anasema mkazi wa kijiji hicho, Mussa Magaigwa ambaye pia ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kerende.

Naye Diwani wa Kata ya Kemambo, Rashid Bogomba, anasema ujenzi wa Shule ya Msingi Mgosi katika kijiji cha Kerende ni sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi mipya inayofadhiliwa na Mgodi wa Barrick North Mara kupitia mpango wake wa CSR.


“Kazi inaendelea vizuri, fedha za CSR zimejenga shule mpya ya msingi Mgosi na majengo yote yamekamilika, haya ni maendeleo makubwa,” anasema Bogomba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika Mgodi wa Barrick North Mara.


Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Mgodi wa North Mara umetumia shilingi bilioni 26.86 kufanikisha utekelezaji wa miradi ya CSR 255 katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tangu mwaka 2019  Barrick ilipoanza kuendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Kupitia utekelezaji wa mradi huu na mingine ya kijamii, Barrick North Mara inaendelea kudhihirisha kuwa uwajibikaji katika uchimbaji madini ni zaidi ya  kuendeleza rasilimali—unahusu kuwekeza kwa watu, kuimarisha jamii, na kusaidia kujenga mustakabali imara zaidi kwa vizazi vijavyo.

Miradi mikubwa ya CSR iliyofanikishwa na Barrick North Mara iko katika sekta ya elimu,maji safi kwa wananchi,afya,ujenzi wa miundombinu ya barabara na uwezeshaji wananchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464