Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania wote kujitokeza na kujisajili katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote akisisitiza kuwa uendeshaji wake unategemea jamii nzima badala ya kuchukuliwa kama mfuko maalum wa kuwasaidia watu wasiojiweza pekee.
Alisema hayo akijibu swali bungeni Dodoma kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Nasriya Nasir Ali, kuhusu mpango wa serikali kuwawezesha watu wenye ulemavu kunufaika na huduma hiyo.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa serikali imeanza rasmi utekelezaji wake tangu Januari mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Alisema serikali imeshatenga fedha za awali za zaidi ya Shilingi bilioni 48 hadi bilioni 50 kwa ajili ya makundi yasiyo na uwezo, huku ikiendelea kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kuongeza wigo wa wananchi watakaonufaika.
Akitofautisha mpango huo na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Dk Mwigulu alisisitiza kuwa mafanikio ya Bima ya Afya kwa Wote yanahitaji ushiriki mkubwa wa wananchi wote kwa kuchangia bima hiyo ili kujenga mfumo jumuishi usiomwacha mtu nyuma.
Alisema uzoefu wa nchi nyingine unaonyesha kuwa mfumo unaotegemea serikali pekee kugharimia huduma kwa wananchi wote haujafanikiwa kikamilifu, jambo ambalo linafanya ushiriki wa wananchi kuwa nguzo muhimu ya uendelevu.
Hivyo, aliwataka viongozi na wabunge kuendelea kuhamasisha jamii ili kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki katika mpango huo na kupata uhakika wa matibabu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
