` UJENZI WA MATANGI YA MAFUTA BANDARI YA DAR ES SALAAM WAFIKIA ASILIMIA 52

WANDAMAN HOTEL

UJENZI WA MATANGI YA MAFUTA BANDARI YA DAR ES SALAAM WAFIKIA ASILIMIA 52


Ujenzi wa matangi 15 ya kisasa ya kuhifadhi mafuta katika eneo la Kigamboni kupitia Bandari ya Dar es Salaam umefikia asilimia 52 na unatarajiwa kukamilika Machi mwakani kwa gharama ya Sh bilioni 678.

Mradi huu unalenga kuhakikisha usalama wa nishati nchini na kushusha bei za mafuta kwa kumaliza gharama za meli kusubiri nje ya bandari, unatekeleza maagizo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan aliyeelekeza kuimarishwa kwa akiba ya kimkakati ya hifadhi ya mafuta ili kujilinda dhidi ya misukosuko ya kimataifa.


Akizungumza wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Bandari hiyo, Abeid Gallus, alieleza kuwa matangi hayo yenye uwezo wa kupokea lita milioni 378 kwa wakati mmoja yatajumuisha mafuta ya dizeli, petroli, na mafuta ya ndege.


Aidha kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa meli za mafuta kukaa bandarini kutoka siku 22 hadi siku saba na muda wa kuhudumiwa kwenye gati kutoka siku saba hadi siku moja.


Sambamba na uwekezaji huo wa nishati, ongezeko la ufanisi wa bandari hiyo kupitia kampuni za uendeshaji kama DP World na TEAGTL kumeuwezesha mzigo kufikia tani milioni 33.7 kwa mwaka 2025/26, huku mamlaka ikilenga kufikisha tani milioni 62 ifikapo mwaka 2031 kupitia ujenzi wa magati mapya, yadi ya Kurasini, pamoja na matumizi ya bandari kavu za Kwala, Morogoro, Isaka na usafirishaji wa mizigo kwa Reli ya Kisasa (SGR) ili kuondoa msongamano wa malori na kuongeza kasi ya usafirishaji wa shehena kwa nchi za ndani na jirani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464