` UJENZI WA MARIDHIANO YA KIMATAIFA : WADAU WATOA SHARTI LA UKWELI NA USHIRIKISHWA

WANDAMAN HOTEL

UJENZI WA MARIDHIANO YA KIMATAIFA : WADAU WATOA SHARTI LA UKWELI NA USHIRIKISHWA



Wakati serikali ikijiandaa kuunda Tume ya Maridhiano ili kuendeleza mazungumzo ya kisiasa na kuweka mazingira ya kufikia mwafaka wa kitaifa kufuatia matukio ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, wadau wa haki, amani na habari wameelekeza kuwa mchakato huo haupaswi kuwa wa maneno matupu, bali ujengwe katika msingi thabiti wa ukweli, uwazi, haki na ushirikishwaji mpana wa makundi yote ya kijamii.

Pendekezo hilo linakuja kufuatia tamko la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kutangaza kuundwa kwa tume hiyo ili kushughulikia masuala ya maridhiano na kuelekea katika hatua za uboreshaji wa katiba, sambamba na kazi inayoendelea kufanywa na Tume ya Uchunguzi wa Jinai iliyochunguza matukio yaliyotokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakizungumzia mchakato huo, viongozi wa asasi za kiraia na vyombo vya habari wameeleza mikakati na masharti ya kufanikisha uponyaji wa vidonda vya taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, Dk. Rose Reuben, amesema kuwa hatua ya kwanza ni kuhakikisha tume itakayoundwa inawakilisha wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu huku ikiondoa mijadala ya mihemko.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania, Ernest Sungura, amesisitiza kuwa maridhiano ya kweli yanajengwa katika msingi wa ukweli na uwazi, huku akitaka vyombo vya habari viwakilishwe na wanahabari wajengewe mazingira salama ya kuripoti.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga, amesisitiza kuwa mchakato huo unapaswa kuwashirikisha wanasiasa, asasi za kiraia, vyombo vya dola, na familia za waathirika, huku uwajibikaji ukichukuliwa kwa waliokiuka sheria ili kurejesha imani ya jamii.

Msimamo huo unaungwa mkono na viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo viongozi wake kama Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Stephen Wasira, wamekuwa wakisisitiza kuwa maridhiano hayapaswi kuwa suala la vyama vya siasa pekee bali yawahusishe Watanzania wote wakiwemo viongozi wa dini na wadau mbalimbali.

Hivyo, wakati ripoti ya Tume ya Uchunguzi ikitoa mwanga wa kuelekea maridhiano na uboreshaji wa katiba, jicho la Watanzania lipo katika namna Tume hiyo itakavyoundwa, hadidu za rejea zitakavyowekwa, na jinsi itakavyotumia fursa hiyo kujenga Tanzania moja imara yenye amani na mshikamano wa dhati.





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464