` TRA: TUTAWASAIDIA WACHIMBAJI KUPUNGUZA MRUNDIKANO WA KODI, RIBA

WANDAMAN HOTEL

TRA: TUTAWASAIDIA WACHIMBAJI KUPUNGUZA MRUNDIKANO WA KODI, RIBA

 

Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Maro akizungumza na viongozi wa wachimbaji wadogo wa madini mgodi wa Mwakitolyo Wilaya ya Shinyanga

Na Stella Herman, Shinyanga

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imewapatia elimu viongozi wa wachimbaji wadogo wa madini katika Mgodi wa Mwakitolyo, Wilaya ya Shinyanga kuhusu taratibu za ulipaji kodi pamoja na changamoto zinazowakabili katika kutekeleza wajibu huo.

Elimu hiyo imelenga kuwajengea uwezo viongozi hao kuhusu taratibu mbalimbali za kodi, huku wakipewa fursa ya kueleza changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao hususani zinazohusu ulipaji wa kodi.

Akizungumza wakati wa semina hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Maro amesema sekta ya madini inaendelea kukua kwa kasi jambo ambalo limeifanya Mamlaka hiyo kuwafikia wachimbaji na kuwapatia elimu ili waweze kutimiza wajibu wao wa kuchangia pato la Taifa.

Amesema TRA itaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji mara kwa mara kutokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa uelewa kuhusu masuala ya kodi, akieleza kuwa Mamlaka hiyo imejikita katika kutoa elimu na huduma wezeshi zitakazowasaidia wafanyabiashara na wachimbaji kutekeleza shughuli zao kwa urahisi.

“Mambo tuliyoyabaini ni uwepo wa mrundikano wa kodi na riba mbalimbali kutokana na kutowasilisha taarifa TRA kupitia vikundi mbalimbali, tumewaelimisha na kuwataka kutoogopa, kwa sababu Mamlaka itawasaidia kujaza ritani zao na kuwawezesha kupata msamaha wa riba ili waendelee kulipa kodi kwa hiari,” amesema Maro.

Afisa mkuu msimamizi wa kodi Mkoa wa Geita Justine Katiti

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wachimbaji Wilaya ya Shinyanga, Elias Amos, amesema elimu hiyo imewasaidia wachimbaji kuongeza uelewa kuhusu masuala ya ulipaji kodi, hatua ambayo amesema itasaidia kupunguza usumbufu katika kutekeleza wajibu huo.

Amesema baadhi ya wachimbaji bado hawana namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN), hali ambayo imekuwa ikiwaletea changamoto wakati wa kutekeleza wajibu wao wa kodi kwa kukosa utambulisho unaowatambua moja kwa moja kama walipa kodi.

Amesema suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na TRA ili kuhakikisha wachimbaji wanapata utambulisho huo na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ya kikodi.

Aidha, Amos amesema hapo awali wachimbaji wengi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya kodi, hali iliyokuwa ikisababisha sintofahamu, lakini elimu iliyotolewa na TRA imeongeza uelewa wao na inatarajiwa kusaidia kuongeza ushiriki wao katika ulipaji wa kodi na kuchangia ukuaji wa mapato ya Taifa.


Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Maro akizungumza na viongozi wa wachimbaji wadogo wa madini mgodi wa Mwakitolyo Wilaya ya Shinyanga










Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464