` TANZANIA YAANGAZIWA KIMATAIFA: YAPELEKA AJENDA YA BAJETI INAYOZINGATIA JINSIA DOHA, QATAR

WANDAMAN HOTEL

TANZANIA YAANGAZIWA KIMATAIFA: YAPELEKA AJENDA YA BAJETI INAYOZINGATIA JINSIA DOHA, QATAR

TANZANIA imeendelea kujitengenezea taswira nzuri katika medani za kimataifa baada ya kuonesha mfano wa kuigwa katika kuimarisha bajeti inayozingatia jinsia (Gender-Responsive Budgeting - GRB) kama nyenzo muhimu ya kuchochea maendeleo jumuishi ya miundombinu.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akielezea uzoefu wa nchi katika kuandaa bajeti inayozingatia misingi ya kijinsia kwenye mjadala maalumu ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB). Mkutano huo uliobeba kauli mbiu ya “Ufunguaji wa Fursa za Miundombinu Inayozingatia Jinsia,” ulifanyika kando ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa AIIB wa 2026 mjini Doha, nchini Qatar.

Akizungumza katika jukwaa hilo la kimataifa, Balozi Omar alieleza kuwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwa kuwa na historia ndefu ya kutekeleza bajeti inayozingatia jinsia tangu mwishoni mwa miaka ya 1990. Alisisitiza kuwa msingi mkuu wa mipango ya Serikali ni kuweka kipaumbele kwa wananchi, jambo ambalo linahitaji uelewa mpana wa demografia ya nchi kupitia takwimu sahihi.
Alifafanua kuwa nchi hutumia sensa ya watu na makazi inayofanyika kila baada ya miaka kumi ili kubaini mwelekeo wa ukuaji wa idadi ya watu na muundo wake, hatua inayosaidia katika kupanga na kutekeleza bajeti kwa ufanisi. 

Aliongeza kuwa bajeti inayozingatia jinsia haimaanishi kutenga bajeti tofauti kwa ajili ya wanawake pekee, bali ni kuhakikisha rasilimali za umma zinapangwa, zinatengwa, na kutekelezwa kwa kuzingatia mahitaji maalum ya jinsia zote.

Katika kuonesha kasi ya mageuzi hayo, Serikali imezindua rasmi taarifa ya bajeti ya kijinsia (gender budget statement) kwa mwaka huu, ambayo inaunganisha hali halisi ya kijinsia na mipango ya bajeti, sambamba na kuanzisha mfumo thabiti wa ufuatiliaji. Licha ya mafanikio hayo makubwa, Mhe. Balozi Omar alikiri kuwepo kwa changamoto zinazohitaji kazi ya ziada, kama vile kuboresha upatikanaji wa takwimu zilizogawanywa kijinsia na kuimarisha uchambuzi wa kina wa masuala ya kijinsia.

Waziri huyo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimkakati na wadau wa maendeleo wakiwemo UN Women na AIIB katika kuleta utaalamu wa kiufundi na uzoefu wa kimataifa. Hata hivyo, alisisitiza kuwa Serikali inapaswa kuendelea kushika usukani na umiliki wa michakato yote ili kuwajibika kikamilifu kwa wananchi, huku akionya dhidi ya mifumo sambamba ya wafadhili inayoweza kuepukwa kwa kuhakikisha misaada inaingia moja kwa moja kwenye mifumo iliyopo ya Serikali.

Mpango mkakati wa Tanzania sasa unalenga kuimarisha mnyororo mzima wa thamani—kuanzia kubaini mapengo ya kijinsia, kuweka vipaumbele vya kitaifa, kupanga bajeti, kubuni miradi, hadi kupima matokeo halisi ya utekelezaji wake.

Kuhusu manufaa ya uanachama, Balozi Omar alibainisha kuwa Tanzania, ambayo iliidhinishwa rasmi kuwa mwanachama wa AIIB mwaka 2023 na kukamilisha mchakato huo mwaka 2025, itaitumia benki hiyo kufadhili miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.

 Alitaja sekta zitakazonufaika kuwa ni pamoja na reli, nishati, na teknolojia za kidijitali, ambapo mazungumzo kati ya pande zote mbili yanaendelea vyema.

Tanzania ni miongoni mwa wanachama wasio wa kikanda (non-regional members) wa benki hiyo yenye jumla ya wanachama 111 kwa sasa, hatua inayozidi kuiweka nchi katika ramani nzuri ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kimataifa.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464